Wakati CCM Ruvuma ikiwatimua wanachama 62 kwa usaliti ikiwamo kumuunga
mkono Edward Lowassa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, wabunge wa chama
hicho wameteua wenzao 15 kufanya tathmini ya uchaguzi huo ikiwamo
mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho.
Katika tukio la
kwanza, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho alisema wamefikia
hatua hiyo baada ya kupokea maoni kutoka kwa wanachama kupitia vikao
kuanzia kata hadi mkoa, na kubaini kuwapo waliokiingiza chama kwenye
matatizo makubwa kutokana na usaliti.
Alisema, hadi sasa
viongozi tisa wametimuliwa wakiwamo wanachama 53 wa kawaida, baadhi
wamepewa onyo kali, wengine walipewa ushauri.
Mwisho alisema mchakato wa kuwawajibisha wengine unaendelea ngazi za juu, kutokana na CCM mkoa kutokuwa na maamuzi nao.
Wabunge
wachunguza
Katika hatua nyingine, chama hicho kimeunda kamati maalumu
ya wabunge 15 kwenda kutathmini uchaguzi huo badala ya kutegemea ripoti
zinazotolewa na makatibu wa wilaya na mikoa pekee.
Hatua hiyo ilifikiwa
juzi mjini Dodoma baada ya wabunge wa chama hicho kukutana na Katibu Mkuu
wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na kukubaliana kuchukua hatua.
Katibu
wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza alisema kamati ya wabunge hao
itawahoji wabunge wote wa CCM 267 kwa kuwa wao ndiyo wahusika wakuu,
kuangalia changamoto walizokutana nazo.
Wajumbe hao 15 ni Joseph
Mhagama, Dk Faustine Ndugulile, Joseph Kakunda, Profesa Anna Tibaijuka,
Mboni Mhita, Peter Serukamba, Innocent Bashugwa, George Mkuchika,
Munira Mustapha, Jasmini Tiisekwa na Abdallah Ulega.
Kamati hiyo
itaangalia mfumo wa kura za maoni kwa wagombea ubunge, ili kuondoa watu
wasiokitumikia chama ambao wamekuwa wakitumia fedha zao kupitia kwenye
kura za maoni.