TAHARUKI imetanda katika eneo la Mashangwa kwenye mpaka wa Narok na Migori baada ya mwanamume kuchinjwa na watu wasiojulikana.
Mwanamume huyo, Jackson Mutito Koirigie alikatakatwa hadi kufa na wavamizi wake.
Naibu kamishna wa Trans Mara Magharibi Bw Mericho Maina alisema haijabainika wazi sababu ya kuuawa kwa mwanamume huyo.
Hata hivyo, alisema maafisa wa polisi wanachunguza kisa hicho kwa lengo la kuwakamata wahusika hao.
“Tunachunguza ili kujua sababu ya kuuawa kwake,” alisema Bw Maina.
Aliwataka wakaazi kuwa watulivu na kutoa habari ambazo zitaelekeza kutiwa nguvuni kwa wahusika.
“Tunaauliza wakazi kushirikiana nasi kwa kutoa habari kwa siri kwa maafisa wa usalama wa ngazi ya juu," alisema.
Chumba cha kulala
Chifu wa lokesheni ya Mashangwa Bw Nick Rioba
alielezea kuwa wavamizi hao walivamia chumba cha kulala cha marehemu
takribani saa nane usiku na kumkata kata kitandani mwake.
Chifu Rioba alisema alifahamishwa kuhusu tukio hilo na
majirani wa marehemu na kuripoti mara moja kwa maafisa wa polisi katika
kituo cha mashangwa.
“Maafisa wa polisi waliandamana nami kwenye eneo la
mkasa na kumpata marehemu tayari amefariki dunia. Wahusika walikuwa
tayari wameondoka na watu walipiga mayowe tu,” alisema.