Msanii wa filamu za kuchekesha, King Majuto amekanusha taarifa ambazo
zilizagaa katika mitandao ya kijamii kwamba amestaafu kuigiza.
Akiongea katika kipindi cha Clouds E cha Clouds TV Jumatano hii, Mzee
Majuto amedai sio kweli kwamba amestaafu kuigiza ila kuna baadhi ya
filamu ambazo hatafanya tena.
“Watu wameniwekea maneno mdomoni, sijasema nimeacha kuigiza,” alisema
Majuto.“Wakati nipo Hija mwaka jana nilikuwa nafikiria niache kabisa
kuigiza, lakini baada ya kurudi nikaona nalazimika kuendelea kuigiza ili
nipate pesa za kuendesha maisha yangu, kwa sababu bila filamu nitakufa
njaa,”
Pia muigizaji huyo amesema hafanyi tena stand up comedy kwa kuwa
wakati anafanya kuna matukio ambayo yatakuwa yanaendelea katika ukumbi
ambayo dini yake hayaruhusiwi.
Pia Majuto amewataka mashabiki wa filamu zake kuendelea kusubiria kazi zake ambazo atakuwa anaandaa mwenyewe.