Hatimaye
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia
Ackson ametoa maamuzi kuhusu hoja ya wabunge kulipwa posho au kutolipwa
wanapoingia Bungeni na baadae kutoka nje kwa shughuli zisizo za Kibunge.
Akisoma
muongozo wake muda mfupi kabla ya kuahirisha kikao cha Bunge jioni hii
baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango kusoma Bajeti
Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, Dk. Tulia alisema kuwa
wabunge wanaofanya vitendo hivyo hawatalipwa posho.
Alitoa
uamuzi huo baada ya kurejea kanuni za Bunge akitumia kanuni ya tano
fasili ya kwanza ya toleo la mwaka 2006 na maamuzi yaliyowahi kufanywa
na Spika waliotangulia katika hali kama hiyo.
“Hivyo
basi, kwakuwa jambo hili halikubaliki, na kwakuwa miongozo kadhaa
imeshatolewa kuwasihi waheshimiwa Wabunge wasitoke nje ya ukumbi wa
Bunge kwa shughuli zisizo rasmi.
"Naagiza
kwamba wabunge wote wanaojisajili kisha kutoka ukumbini kwa kususia
vikao vya Bunge, hawatastahili kulipwa Posho kwa siku zote ambao
wamekuwa wakijisajili kuingia ukumbini na kisha kutoka ukumbini,” alisema Naibu Spika.
Wabunge
wa Upinzani wamekuwa wakitoka nje ya Bunge muda mfupi baada ya kuingia
Bungeni katika vikao vyote vinavyoongozwa na Naibu Spika kwa madai kuwa
hawana imani naye kwakuwa amekuwa akiongoza Bunge kwa ubabe na
kuwapendelea wabunge wa CCM.