MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Iringa imesema mtuhumiwa wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti
wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, Daudi Mwangosi, ana kesi ya
kujibu.
Mtuhumiwa
huyo Pacificius Cleophace Simoni alifikishwa mahakamani hapo akituhumiwa kumuua
Mwangosi kwa kukusudia katika tukio lilitokea katika kijiji cha Nyololo,
wilayani Mufindi Mkoani Iringa Septemba 2, 2012.
Akitoa
uamuzi huo jana, Jaji wa mahakama hiyo, Paul Kiwelo alisema; “Mahakama
imejiridhisha kwamba katika shauri lililoko mbele yetu, tuhuma ambazo
zimetolewa dhidi ya mtuhumiwa na kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na upande
wa Jamuhuri, mtuhumiwa ana kesi ya kujibu kwahiyo natupilia mbali ombi la
upande wa utetezi lililotaka kesi hii itupiliwe mbali kwa madai kwamba hakukuwa
na ushahidi wa moja kwa moja unaomuhusisha mtuhumiwa na mauaji hayo.”
Jaji
Kiwelo alisema mtuhumiwa huyo ataanza kujitetea leo baada ya kuridhia ombi
hilo lililotolewa na wakili wa upande wa utetezi Lwezaula Kaijage na kuungwa
mkono na mawakili wa Jamuhuri, Sandy
Hyra na Ladslaus Komanya.
Mara
baada ya Jaji huyo kutoa uamuzi huo, askari Polisi zaidi ya 20 waliokuwa ndani
ya chumba cha mahakama hiyo, walimfunika shuka mtuhumiwa huyo ili wanahabari
wasipate fursa ya kumpiga picha.
Mtuhumiwa
huyo alitolewa mahakamani hapo na kundi la askari hao, akiwa amefichwa katikati
yao, hatua ambayo pia iliwazuia wanahabari kufanya kazi yao vizuri.
Tofauti
na watuhumiwa wengine, mtuhumiwa huyo aliyekuwa askari wa FFU Iringa kabla ya
kufikishwa mahakamani hapo aliondolewa katika eneo la mahakama kwa kutumia gari
dogo la Polisi aina ya Landlover badala ya kupandishwa katika kalandinga kama
inavyofanywa kwa watuhumiwa wengine.
Kabla
na baada ya kesi hiyo kusikilizwa baadhi ya wanahabari walilalamika kwa Msajili
wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Ruth Massam namna baadhi ya askari waliokuwa
wamevaa kiraia na sare za jeshi hilo walivyokuwa wakiwatisha wakati wakiwazuia
kupiga picha.
Wanahabari
hao walilalamika kwamba kila kesi hiyo inapofikishwa mahakamani hapo, kumekuwa
na kawaida ya kuwepo kwa idadi kubwa ya askari wanaovaa kiraia na wale wanaovaa
sare, huku baadhi yao wakiwa na silaha za moto jambo ambalo pia linawaogopesha
na kuwakwamisha kufanya kazi zao kwa staha.
Akizungumzia
malalamiko hayo, Msajili huyo alisema mahakama inaendelea kuyafanyia kazi huku
akisisitiza shughuli za kimahakama ni shughuli zao ambazo hazipaswi kuingiliwa
na mtu mwingine na kwamba atazungumza na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa
ili asaidie kutoa maelekezo kwa baadhi ya askari wake wanaotaka kuingilia uhuru
wa mahakama