Siku moja tu baada ya serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi
na usalama nchini kuahidi kuwasaka watu waliofanya mauaji ya kutisha kwa
kuwachinja watu nane wa mtaa wa Kibatini uliopo kata ya mzizima jijini
Tanga, operesheni ya majeshi hayo imeanza katika maeneo mbalimbali hasa
katika pori la Mleni maji moto ambalo linadaiwa kuwa ni sehemu ya
maficho ya wahalifu.
Blog hii imeshuhudia askari wa majeshi wakizingira mapori ya Mleni maji
moto yaliyozunguka kijiji cha Kibatini huku baadhi ya wakazi wa mtaa huo
wakiiomba serikali kuwahamisha haraka katika eneo hilo au kuendelea
kuimarisha ulinzi kwa wananchi kwa sababu baadhi ya wananchi wameanza
kuhama na kukimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wao.
Baadhi ya wakazi waliopo katika eneo la Amboni wamelalamikia kuwepo
kwa mapori makubwa ya mashamba yanayodaiwa kuhifadhi wahalifu, na
kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwapa wakazi wanaohangaikia
maeneo ya kilimo pamoja na wawekezaji wenye uwezo wa kuyaendeleza kama
ilivyokuwa kampuni ya Amboni hapo awali.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya wakuu wa majeshi ya ulinzi na
usalama wakiongozwa na naibu waziri wa mambo ya ndani Hamad Masauni
kwenda kuwapa pole wafiwa kisha wakuu wa majeshi hayo wakiahidi kuwasaka
watuhumiwa waliohusika na mauaji ya kikatili dhidi ya watu nane akiwemo
mjumbe wa serikali ya mtaa wa Kibatini ambao walichinjwa na watu
wasiojulikana.