Hofu ni kuwa paka hao wanaashira kumwagwa katika eneo
hilo na watu wanaoabudu mashetani huku kukipangwa maombi maalum wikendi
ijayo kumuomba mwenyezi Mungu aingilie kati katika hali hiyo wanayoitaja
kuwa ya kuogofya.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko la
Kangari Bi Mary Wachiuri, kufikia Jumatano asubuhi kulikuwa na visa
vitano vya paka hao kuonekana na kushambulia watoto wawili, mwanamume
mmoja na wanawake wawili na wote ambao wameachwa na majeraha ya kuumwa.
“Paka hao wanaposhambulia wanalenga tu miguu na wote
walioathirika na uvamizi wao wako na majeraha yanaoanzia magoti
kuteremka chini hadi kwa kisigino. Hatuelewi ni kwa nini hawalengi
popote pengine ila tu miguu ya binadamu,” akasema.
Akiongea na waandishi wa habari katika mji huo, Bi
Wachiuri alisema kuwa paka hao wanakisiwa kuwa wawili na wenye rangi
nyeusi na ni kama wametumwa katika eneo hilo na mwenyeji mmoja ambaye
anakisiwa kuwa mfuasi sugu wa imani ya kishetani.
“Mtu huyo ni mwanasiasa na kila wakati tunapokaribia
uchaguzi, paka hao huwa wanajitokeza na huwa wanaandamana na ajali za
barabarani katika eneo hili. Katika kipindi cha wiki moja sasa, kando
na majeraha hayo kwa watu watano mikononi mwa paka hao, kuna ajali
takriban 12 zikihusisha pikipiki na pia magari katika mji huu wetu.
Tunaishi kwa hofu kuu,” akasema.
Bi Wachiuri aliteta kuwa wameripoti kisa hicho kwa
maafisa wa polisi lakini wakaagizwa wawe macho wajikinge kwa kuwa “kazi
ya kusaka wanyama imo mikononi mwa idara ya wanyama pori.”
Aliteta kuwa maafisa hao hawaonekani kutambua kuwa
hatari iliyoko ni kama ya uvamizi wa mizimu na wanafaa kuchukulia suala
hilo kama “vita dhidi ya jamii na adui anayejifananisha nap aka huku
akiwa ni binadamu.”
Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Murang;a Bi Naomi
Ichami alisema kuwa “hali hiyo ni ya kushangaza na tayari tumepokezwa
ripoti kuihusu.”
Kukaa macho
Alisema kuwa maafisa walio katika eneo hilo wameagizwa
wakae macho na wakiona paka yeyote akishambulia binadamu akabiliwe kwa
nguvu inayostahili.
“Lakini ni hali ya kushangaza bado nasisitiza kwa kuwa
ni kisa cha kipekee. Tunajua kuwa wanyama wengine wanaofugwa na jamii
huingiwa na kichaa na kuishia kushambulia binadamu lakini taarifa
tunazopokezwa zinatia shaka kuhusu hali hiyo. Lakini tutawajibika na
kuandaa doria za kina tukisaka adui huyo wa kipekee. Lakini bado
tunasisitiza kuwa wenyeji wamgeukie Mungu ili awatulizie shaka zao
kuhusu Imani ya kweli na ile ya kujitwika pasipo uhakika,” akasema.
Alisema kuwa maafisa wake watasaka paka hao na
akawaomba wenyeji wakiwaona wapige ripoti mara moja “ili hata maafisa
wetu wajifahamishe na maumbile ya paka hao na watekeleze utathimini wao
wa kina kuhusu kama ni wa kweli au ni wa kutumwa kutoka kuzimuni,”
akasema.