Mtoto afariki wakati aking'ang'aniwa na wazazi wake

MTOTO mwenye umri wa miaka miwili aliaga dunia Alhamisi asubuhi wakati wazazi wake waliokuwa wametengana walipokutana ghafla barabarani na wakaanza kumng’ang’ania katika kaunti ya Kirinyaga.

Kisa hiki kilitokea katika eneobunge la Gichugu katika kijiji cha Kathange na kuwaacha wenyeji katika mshangao mkuu.

Kwa mujibu wa afisa Mkuu wa Polisi wa eneo hilo Bw Rono Bunei, wawili hao walikutana na ubishi ukazuka huku bwana akimtaka mwanaye naye mamake akimkatalia.

“Kwa hasira, mwanamume huyo kwa jina Peter Mugo alichukua kigongo akinuia kumgonga mamake mtoto lakini kwa bahati mbaya akakihepa na kikaishia kumwangukia mtoto huyo kichwani hivyo basi kumuua papo hapo,” akasema.

Wawili hao walikuwa wameachana miezi kadhaa iliyopita lakini siku ya mkasa, mwanamume huyo alikuwa katika harakati za kumnyemelea mtoto wake ili amtwae aende kuishi naye.

Kulingana na mamake mtoto huyo, Bi Alice Muthoni, walitengana kufuatia kukosa uwajibikaji wa kifamilia na pia ulevi kwa upande wa mumewe huyo.

Kutaka mtoto

“Mimi niliamua kurudi kwetu ili nianze maisha upya huku nikimlea mwanangu. Lakini ghafla mwanamume huyo alijitokeza na akadai anamtaka

mwanaye. Kama nimjuavyo, hawezi akawachiwa wajibu wa kulea mwana,” akasema.

Mwanamume huyo alikamatwa na anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kerugoya akingojea kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.

“Ni kisa cha kusikitisha huku mwanamume huyo akionekana kujutia hasira zake. 

Lakini sheria lazima idumishwe na hata ikiwa alimuua mtoto huyo bila kukusudia, hakuna vile tutakosa kuwajibikia haki na tutamwasilisha mahakamani akajitetee huko punde tu uchunguzi wetu utakapomalizika,” akasema Bw Bunei.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo