TAARIFA KWA UMMA KUTOKA KWA MSTAHIKI MEYA BONIFACE JACOB
Asalaam aleikum wananchi wa wilaya ya kinondoni na viunga vyake,
niendelee kuwaombea ndugu zetu waislamu funga yao iwe na heri na baraka
tele ikiwa leo ni chungu cha 19.
Leo tarehe 25 june 2016,
nimepigiwa simu nyingi sana na kupokea taarifa kwa njia mbalimbali,
nikiulizwa nilipo? kwanini sipo kwenye tukio la Biafra la uzinduzi wa
shughuli ya jeshi la polisi? na wengine wakiniuliza neno baada ya
kuuliziwa hadharani na mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa
Tanzania.
MHESHIMIWA RAIS John pombe Magufuli; Mstahiki meya
manispaa ya kinondoni leo siku ya jumamosi kijana wako na mtumishi wa
wananchi wa manipsaa ya kinondoni nilikuwa naunga mkono shughuli za
usafi. Nimeshinda na wananchi wa ubungo kisiwani kutwa tukifukua mitaro
ya maji machafu kuhakikisha usalama wa afya za ubungo kisiwani zipo
salama na zaidi kuweka miundo mbinu yetu sawa.
Nami nilitamani
sana kukuona japo kwa karibu sana au kuongea na wewe mambo kadhaa kwa
mustakabali wa kinondoni yetu na nchi yetu kwa ujumla, hasa hali ya
kisiasa na kiuchumi ili kurahisisha upatikanaji wa Maendeleo.
Mheshimiwa Rais leo nadhani umejionea mahusiano yenye shaka na mabaya
niliyokuwa nalalamikia siku zote kwa njia mbalimbali. Viongozi wa wilaya
na mkoa hatuna tena ukaribu wakupashana wala kutaarifiana habari
yoyote,
iwe nzuri au mbaya.
Mheshimiwa Rais, meza kuu
ilipaswa kukwambia ama kukupa jibu kuwa sikuwa na mwaliko leo wa
kuhudhuria shughuli hiyo hakuna kiongozi wa polisi yeyote ,awe IGP, RPC,
OCD wala OCS aliyenipigia simu au kunitumia unumbe wa aina yeyote kuwa
nikaribie tukio lako la leo. Hakuna mjumbe wa kamati ya ulinzi na
usalama ya mkoa wala wilaya aliye nitumia ujumbe wa aina yeyote au
kinipigia simu akinijulisha au kuniomba nikaribie kwenye tukio lako leo.
Mheshimiwa Rais; shughuli za ulinzi na usalama zina taratibu zake, na
mimi mstahiki meya wa kinondoni siyo mjumbe wa kamati ya ulinzi, kuanzia
mtaa, kata, wilaya mpaka mkoa. Hivyo ni ngumu sana kujua shughuli hizo
wala kuhusishwa kama haujapewa taarifa na wahusika walioandaa ujio wako
na uzinduzi wa leo.
Mheshimiwa Rais, binafsi nilichukulia kwa
uzito kuwa sihitajiki mahala hapo kwakuwa tukio lako la leo nilishatoa
ushirikiano kabla ya kuona sina mualiko, kwakuwa greda la kusafisha na
kuandaa eneo la tukio lako nili idhinisha mimi na kuhakikisha polisi
wanapatiwa kutoka kwa wananchi wa kata ya Goba lilipo kuwepo likikwangua
barabara.
Baada ya ombi lao la greda kufanikiwa kusafisha
vizuri, Juzi siku ya alhamisi, karani wangu alipokea barua maalum yenye
malekezo maalumu yakitaka madiwani watano waje kwemye shughuli hiyo.
Barua hiyo maalumu yenye mihuri ya siri niliitekeleza kwa kuteua
madiwani watano tena kutoka kwenye kamati ya fedha,nilijua ni taratibu
tuh za kiusalama, ambapo leo walihudhuria. Laiti barua hiyo ya polisi
ingenitaja tuh au kama ningetumiwa barua yangu binafsi basi
ningehudhuria tukio hilo bila shaka.
Mheshimkwa Rais,binafsi
nimeshindwa kulielewa jeshi la polisi kama ulivyoshindwa kunielewa mimi,
kwakuwa bado ninaamini kuwa pamoja na makandokando ya kisiasa yaliyopo
walipaswa kunialika. Si mimi tu, bali pamoja na viongozi wengine wa
upinzani kwakuwa zoezi hili lilikua ni lakitaifa.
Mheshimiwa
Rais nimalize kwa kusema kuwa laiti ninge pata mualiko ningefika kwa
heshima yako kwakuwa naamini bado kinondoni inahitaji mahusiano bora
baina ya manispaa ya kinondoni na serikali kuu. Jambo la leo
lilitawaliwa na baadhi ya watendaji kusutwa na dhamira zao, kuona
ningekaaje meza kuu mimi meya wa upinzani, ndiyo maana sikuwa meza kuu
na kiti changu,wala rasimu ya ratiba ainitaji popote wala kunipa walau
nafasi ya kusalimia,ukiondoa nia yako njema binafsi ya kunitambua,kwao
waliona sistahili na hakuna haja hiyo ya kuapata wasaa au heshima wakati
wamejipa kazi kuua demokrasia ambapo mimi ni tunda la siasa za vyama
vingi.
Mheshimiwa Rais, binafsi nina historia ngumu sana ya
kuonja machungu ya jeshi la polisi kama walivyo wapinzani wote. Ila
kwenye maendeleo wakinihitaji wakati wowote,nitatoa ushirikiano wangu
kwa nguvu na akili zote, ndiyo maana tumekuwa tukisisitiza *polisi
wasitupige mabomu chadema ni serikali ijayo*.
ASANTENI,
IMETOLEWA TAR 25/6/2016
NA MSTAHIKI MEYA WA MANISPAA YA KINONDONI: BONIFACE JACOB
