Aliyemuua Matonya jela miaka mitano
MAHAKAMA Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imemhukumu Baraka Hopaje
(26) kwenda jela miaka mitano baada ya kupatikana na hatia ya kosa la
kumuua Majuto Matonya bila kukusudia.
Pia, mahakama hiyo imeagiza mshtakiwa aendelee kupata huduma
ya chakula maalumu pamoja na dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs)
kama alivyoandikiwa na daktari.
Jaji alisema baada ya kupitia hoja zilizotolewa na pande
zote mbili, ikiwemo maelezo ya onyo ya mshtakiwa aliyoyatoa wakati
akihojiwa polisi pamoja na ombi lake la mazingira rafiki ya kutumia dawa
na chakula pamoja na miaka minne aliyokaa mahabusu, smhtakiwa huyo
aliomba kupunguziwa adhabu.
Pia, mahakama imesikiliza hoja za Jamhuri kwamba mshtakiwa
amefupisha maisha ya Matonya na kwamba amekufa na kuacha familia
iliyokuwa ikimtegemea hivyo mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho.
Jaji alisema kwa sababu mshtakiwa alitoa ushirikiano
alipohojiwa na polisi lakini kitendo cha kukatisha uhai wa Matonya
hakiungwi mkono pamoja na kukaa mahabusu miaka minne atakwenda jela
kutumikia kifungo cha miaka mitano
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Agosti 12, mwaka 2011
katika baa ya Mashujaa mshtakiwa akiwa kazini kama kaunta wa baa hiyo
alimuua bila kukusudia Matonya baada ya kutokewa ugomvi uliosabishwa na
wivu wa mapenzi.
