Watu wawili mume na mke wameuawa kwa
kuchinjwa shingo na watu wasiofahamika wakati wakiwa
wamelala nyumbani kwao usiku wa kuamkia jana katika kijiji cha Mmazami Kata ya Bukabwa Wilaya ya Butiama Mkoani Mara.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Jackson Kitukuru
amewataja waliouawa kuwa ni Saidi Somba(48) na mke wake
Kadogo Ehicho(47) wote wakazi wa kijiji cha Mmazami.
Kitukuru amesema tukio hilo la kusikitisha lilitokea usiku wa manane wakati wanafamiliya hao
wakiwa wamelala na kwamba, watu hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi walifungua mlango
bila wanafamilia kusikia chochote kwa kupitisha mkono katika tundu lililo jirani na komeo la mlango kwa ndani.
Amesema baada ya kufanikiwa kuingia ndani walimchinja kila mtu shingo mithili ya kuchinja mnyama nao mwanamke alichinjwa kwa mbele (kwenye koromeo) wakati mwanaume alichinjwa
shingo kwa nyuma.
Kitukuru amesema wakati na baada ya mauaji hayo hakuna mtu wala jirani aliyeweza kutambua
tukio hilo hadi ilipofika saa mbili asubuhi baada ya mtoto wa marehemu hao aliyekuwa amelala
nyumba nyingine kuingia katika nyumba ya wazazi wake kwa lengo la kuwaamsha baada ya kuona
hawaamuki.
“Huyu mtoto ameamka asubuhi, ameenda kwenye shamba lao la mpunga kuangalia ndege,
amerudi, akaona kimya akaamua kuingia ndani baada ya kuona mlango upo wazi, lakini hakuna
anayeongea akakutana na damu nzito, huku wazazi wamechinjwa,” amesema Katukuru