Mlinzi akamatwa kwa kuiba nyumbani kwa Mkuu wa wilaya

Polisi mkoani Singida wanamshikilia Saidi Abdallah (49), ambaye ni mlinzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Cosmas Pascal kwa tuhuma za kuvunja nyumba ya mwajiri. 

Abdallah anadaiwa kuiba mali mbalimbali, ambazo kwa sasa thamani yake haijafahamika. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka alisema tukio hilo limetokea juzi saa 12.00 jioni Manyoni Mjini. 

Sedoyeka alisema siku ya tukio, mkuu wa wilaya alipigiwa simu na mlinzi wake huyo akimweleza kuwa nyumba yake imevunjwa mlango wa mbele na vitu mbalimbali vimeibwa. 

Alisema baada ya Pascal kupigiwa simu aliwaarifu polisi ambao walifika eneo la tukio na kukuta mlango umevunjwa, hivyo wanamshikilia mlinzi huyo kwa ajili ya kuwasaidia kwenye upelelezi. 

Katika matukio mengine, Sedoyeka alisema watu wawili wamefariki dunia kwenye matukio mawili tofati likiwamo la kifo cha dereva wa lori aina ya Fuso, Bakari Alli (32) ambaye haijajulikana anakotokea. 

Alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 11.00 jioni wakati Fuso hilo likiteremka Mlima Saranda wilayani Manyoni, liligonga basi aina ya Dargon linalomilikiwa na Kampuni ya Leo Luxury Coach na kwamba, Bakari alishindwa kulimudu kutokana na kufeli breki. 

“Bakari alifariki papo hapo na abiria mfanyabiashara mkazi wa Kibaha, Richard Dominick (40) alivunjika mkono wa kulia amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni,” alisema Sedoyeka. 

Pia, alisema katika ajali nyingine iliyotokea juzi saa 2.00 usiku Mtaa wa Majengo Manyoni Mjini, mwendesha pikipiki aina ya Fekon, Riziki Samson (26) amefariki dunia baada ya kugongwa na semi trela lilokuwa likivutwa na lori aina ya Scania, lililokuwa likiendeshwa na mkazi wa Arusha Mjini. 

Alisema mwili umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti Hospitali ya Mkoa wa Singida kwa uchunguzi, baadaye utakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko. 

Sedoyeka alisema chanzo cha ajali hiyo, ni uzembe wa dereva wa lori ambaye alikuwa akijaribu kupita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine. 

Alisema wanamshikilia dereva wa lori baada ya kumaliza mahojiano, watamfikisha mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili. 

Kamanda Sedoyeka aliwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kwamba, kila mtu ana haki.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo