Wakazi wawili jijini Dar es Salaam
wamehukumiwa vifungo vya maisha jela kwa makosa ya ubakaji
na unyang’anyi wa silaha.
Hukumu hizo za kesi mbili tofauti, zilitolewa jana kwenye Mahakama ya Wilaya ya Ilala.
Emmanuel Abdul (22) alihukumiwa kifungo cha maisha jela na
kulipa fidia ya Sh5 milioni kwa kumbaka binti wa miaka saba.
Kesi ya pili ilimhusu mfanyabiashara wa Magomeni, Hamidu Ally (27) ambaye amehukumiwa
kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
Hukumu ya kesi ya kwanza ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Said Mkasiwa na kwamba mtuhumiwa wa ubakaji pia, atalazimika kumlipa fidia ya Sh5 milioni binti huyo ambaye anasoma
darasa la pili.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkasiwa alisema Mahakama yake imeridhishwa na ushahidi
uliotolewa na upande wa mashtaka ikiwamo fomu namba 3 ya polisi (PF3).
Kabla ya kutolewa kwa kuhumu hiyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Sylvia Mitanto
uliiomba Mahakama hiyo kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo, kutokana na kukithiri kwa
vitendo vya ubakaji.
Abdul anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 11, 2014 katika eneo la Ulongoni, Gongo la Mboto.
Kuhusu kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, Hakimu Mkasiwa katika hukumu ya kifungo cha maisha aliyoitoa jana kwa mfanyabiashara huyo, alisema ushahidi ulionyesha ni kinara wa matukio ya uporaji na alikuwa akitafutwa na polisi baada ya kuikimbia mahakama hiyo.
Hakimu Mkasiwa alisema mshtakiwa huyo alikamatwa juzi kwenye Kituo Kikuu cha Polisi,
alikokuwa amekamatwa kwa kosa lingine la uporaji, huku akiwa amendikisha jina jingine tofauti
na jina lake halisi.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Said Mkasiwa alisema Mahakama imemtia hatiani baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi watano.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto, aliiambia Mahakama
kuwa, mtuhumiwa alikuwa na rekodi za nyuma za uhalifu na hivyo kuiomba Mahakama kutoa
adhabu kali ili iwe onyo na fundisho kwa wote wenye tabia kama hiyo.
Mahakama ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea ili asipewe adhabu hiyo, lakini alishindwa na
badala yake aliomba kumpatia tarehe nyingine kuja kujitetea, ombi ambalo lilitupiliwa mbali na mahakama hiyo.