Mama mzazi wa binti mmoja mkazi wa
Dakawa wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro hivi karibuni
alipokea ujumbe wa picha ya video katika simu yake ya mkononi
na haraka aliifungua akiwa na shauku ya kuitazama.
Lahaula! Shauku yake ya kuitazama video hiyo aliyodhani ni
sawa na nyingine za matukio ambazo amekuwa akiziona
zikisambazwa mitandaoni, iligeuka huzuni na fedheha kubwa
alipoona ikimwonyesha bintiye akidhalilishwa na wanaume
huku akilalamika asirekodiwe bila mafanikio.
Mama huyo alijizoazoa haraka na simu yake akatimua mbio
hadi Polisi kuripoti tukio hilo lililolenga kumdhalilisha binti
yake na kuifedhehesha familia nzima. Hicho ndiyo kiini cha
vijana 11 wa Dakawa kukamatwa ili waisaidie Polisi kuhusu walioshiriki tukio hilo na
walioisambaza video hiyo kwa mama huyo na kwenye mitandao ya kijamii hasa WhatsApp.
Katika video hiyo, wakati mwanamme mmoja akimdhalilisha huyo binti, mwingine alikuwa
akirekodi na baada ya kukamilisha tendo hilo lisilo na utu tena bila huruma waliwatumia watu
wengine katika eneo la Dakawa.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Betty Mkwasa aliliambia gazeti la Mwananchi kuwa miongoni mwa watu
wa kwanza kuona video ile alikuwa mama wa msichana. “Alikimbia polisi kwenda kutoa
taarifa,”alisema Betty.
Baada ya kufika Polisi, Betty alisema polisi walimwambia mama huyo hawawezi kuandika maelezo
hadi mhusika ambaye ni binti yake afike kituoni. Walisema hivyo kwa sababu ni mtu mzima hivyo
anatakiwa kutoa maelezo mwenyewe.
Saa chache baada ya kuandikisha maelezo yake, polisi
waliwakamata vijana wawili kwa tuhuma za kuhusika na unyama huo. Betty alisema watuhumiwa
hao walikamatwa juzi na leo watafikishwa mahakamani.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kwamba suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi na kwamba hadi jana watuhumiwa 11 walikamatwa
kuhusiana na tukio hilo.
Kamanda Matei alisema tisa kati yao wanaoshikiliwa ni kwa kosa la kusambaza picha za utupu
huku vijana wawili ambao ni Zuberi Thabiti (30) na Iddy Adamu (32) ni kwa kosa la kufanya mapenzi na msichana huyo kwa nguvu huku wakirekodi.
Ilivyokuwa
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Matei alisema kuwa watuhumiwa hao walifanya kitendo hicho
Aprili 28 mwaka huu majira ya saa 1.00 usiku katika nyumba ya kulala wageni yenye jina la ‘Titii’
iliyopo Dakawa.
Kamanda Matei alisema kuwa binti huyo aliitwa kwenye nyumba hiyo ya wageni na Thabiti
ambaye ni mkazi wa Mbarali wilaya ya Mbeya ambaye alikuwa na uhusiano naye kimapenzi.
Baada ya kuingia chumbani alimkuta pia Adamu mkazi wa Makambako, Njombe ambao
walimlazimisha kufanya mapenzi huku mmoja akimrekodi picha za video na baadaye kuzisambaza
kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Wanaoshikiliwa kwa kosa la kusambaza picha za utupu ni Rajabu Salehe (26), Said Athman (26), Musi Ngai (36), Said Muhammed (24), John Peter (24), Hassan Ramadhan (27), Ramadhan Ally
(26), Lulu Peter (38) na Magreth Njonjone (30).
Wote ni wakazi wa Dakawa, Morogoro na wamevunja Sheria ya Makosa ya Mitandao, kifungu
namba 14, kifungu kidogo (1) (a)
Kamanda Matei alisema wakati wa tukio hilo watuhumiwa hao walimtisha binti huyo kwa kisu ili
asipige kelele wakati akidhalilishwa na walimtaka asitoe siri hiyo vinginevyo watamuua.
Kamanda alisema wawili hao ni marafiki wa msichana huyo na kwamba Thabiti ambaye ni mpenzi wa sasa wa msichana huyo alipanga na Adamu ambaye ni mpenzi wake wa zamani
kumkomesha.
Alisema Thabiti alimwambia mpenzi wake wakutane hotelini. Msichana alipofika aliwakuta
chumbani huku Adamu akiwa ameshika kisu na kamera.
“Wakamlazimisha afanye vile na
kumtishia kumuua kama angekataa,”alisema Matei.
Hata hivyo, Betty alisimulia kisa hicho na kusema watuhumiwa hao walifanya unyama huo kwa
sababu ya usaliti wa mapenzi.
Alisema msichana alidaiwa kujihusisha kimapenzi na dereva wa mpenzi wake.
Kwa mujibu wa Betty, baada ya mpenzi wake kugundua alipanga njama ili kuwakomoa wote
wawili.
Alisema mpenzi wake alimwambia wakutane hotelini na alipofika alimkuta Zuberi pamoja
na dereva wa mchumba wake hotelini.
“Akawambia wafanye kile kitendo huku akirekodi video,”alisema Betty. “Nia yake ilikuwa
kuwakomoa…kwa nini atembee na dereva wake,”alisema Betty na kwamba baada ya hapo picha
hizo zilianza kusambaa.
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk
Hellen KijoBisimba alisema hali hiyo inaonyesha jinsi maadili yanavyozidi kuporomoka katika
jamii.
“Hilo siyo kosa la kisheria peke yake ni udhalilishaji mkubwa,”alisema.
Dk Hellen alisema licha ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu kukemea suala hilo ni vyema jamii ikazingatia suala la maadili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Edda Sanga
alisema vyama vya kutetea haki za wanawake vinafanya mkutano wa pamoja kujadili suala hilo.
“Leo (jana) tumekutana ili tujadili na kuja na tamko la pamoja,”alisema Sanga na kuongeza
kwamba jambo hilo halivumiliki kwa sababu vitendo kama hivyo vinaendelea kujitokeza mara kwa mara.
Chanzo: Mwananchi
