KUTOKANA
na matukio ya udhalilishaji dhidi ya wanawake kuongezeka kwa kasi
nchini, taasisi zinazotetea haki za wanawake na watoto, zimevitaka
vyombo vya dola kuamka na kuchukua hatua za haraka zitakazosaidia
kukomesha matukio hayo
Akizungumza
jana na waandishi wa habari Dar es Salaam Lilian Liundi, Mkurugenzi
Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia (TGNP), akiwa na wanaharakati wengine
alisema kuwa, tangu Januari hadi kufikia Aprili mwaka huu matukio ya
udhalilishaji na unyanyasaji dhidi ya wanawake yamekuwa yakizidi kushika
kasi.
“Tuko
hapa kwa pamoja tukilaani vikali ukatili dhidi ya wanawake unaoendelea
kukithiri nchini, mfano kuna tukio lilitokea hivi karibuni katika mji
mdogo wa Dakawa wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro ambapo binti wa miaka
21 alikuwa akibakwa na picha za video dhidi ya tukio hilo kusambazwa
kwenye mitandao ya kijamii,
“Si
hilo tu bali taarifa tulizozikusanya juu ya matukio ya ukatili wa
kijinsia tangu mwaka huu uanze ni mengi katika kila kona ya Tanzania,
tunaona Aprili mwaka huu Yunis Peter mkazi wa Dar, alichomwa na kitu
chenye ncha kali katika nyumba ya kulala wageni, Rehema Lubinza mkazi wa
Mlele, aliuwawa kikatili kwa kukatwa na mapanga na mumewe kisha mwili
wake kufungiwa ndani, si hivyo bali tukio la muuguzi wa Zahanati ya Kagu
Geita, bi Elizabeth Msango, ambaye aliuwawa na watu wasiojulikanayapo
matukio mengi ambayo ni unyanyasaji unaonekana kabisa”alisema.
Akizungumzia
kuhusu udhalilishaji uliofanywa Mvomero, Gladness Munuo, Mratibu wa
dawati la usuluhishi kutoka chama cha Wahariri Wanawake Tanzania,
(TAMWA), alisema tukio hilo ni kinyume na sheria ya kanuni ya adhabu
sura 16(Kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 ambayo imeainisha
makosa ya kujamiana).
Alisema
pamoja na sheria za ndani, serikali ya Tanzania imeridhia mikataba na
matamko mengi kuhusu haki za wanawake na usawa wa kijinsia ikiwamo
mkataba wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake(CEDAW),
pamoja na mkataba wa haki za watoto (CRC), sambamba na tamko la
kimataifa la haki za binadamu (UDHR,19),ambalo linatambua haki za
wanawake na watoto.
Theodosia
Nshala, Mkurugenzi wa kituo cha msaada wa sheria kwa wanawake (WLAC),
alisema kama kituo tayari wameshapokea kesi kumi na mbili lakini licha
ya kufanya jitihada za kuzishughulikia bado wahusika ama waathirika
wamekuwa wakikata tamaa kutokana na kesi hizo kuchukua muda mrefu ambapo
kesi moja ambayo ina ushahidi uliojitosheleza inaweza kuchukua hata
miaka mitatu mpaka mitano .
Grace
Mwangamila, Mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na haki za
binadamu(LHRC), alisema kupitia tafiti zao matukio ya udhalilishaji
dhidi ya wanawake yameoneka kuwa mengi huku kwa upande wa watoto
udhalilishaji na unyanyasaji umebainika ukifanyika ndani ya familia.
