Mwenyekiti
wa Taifa wa chama cha Tanzania Labour Party ( TLP), Augustino Mrema
amelaani hatua ya Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif kutangaza kumwondoa
Rais wa Zanzibar, Dr Shein madarakani kabla ya 2020 huku akiwataka
wazanzibar kutoyumbishwa na kauli za mwanasiasa huyo.
Mrema
amezungumza hayo leo jijini Dar es salaam mbele ya waandishi wa habari
na kusema kwamba amani ya Zanzibar ni muhimu kuliko maslahi binafsi
hivyo ni vyema kuzitafakari kauli ambazo zinaweza kuleta machafuko.
Amesema
hakuna mtu aliye juu ya sheria hivyo kuwepo kwa watu wanaochochea
vurugu ni kama waahini pia ni vyema hatua zichukuliwe dhidi yao
katika kuhakikisha wananchi wanakuwa salama
Aidha
Mrema amesema kwamba amani ya Zanzibar ikiharibika hata bara haiwezi
kuwa salama hivyo ni vyema kauli za kuvuruga amani zizingatiwe ili
kulinda maslahi ya wananchi wa pande zote mbili.
Amesema
Zanzibar ina historia ya kuuawa watu mwaka 2001 kutokana na vurugu za
kisiasa hivyo lazma kwa sasa suala la ki uchochezi liangaliwe kwa
macho mawili dhidi ya watu wanaotaka kuvuruga amani katika mazingira
hayo.
Mrema
amesisitiza hakuna chama cha siasa ambacho kinajengwa kwa kususia
uchaguzi bali kwa kufanya hivyo ni kuwanyima wapiga kura haki pia ni
hatari na kunaweza kusababisha chama kusambaratika kama kulivyotokea
kwa baadhi ya vyama mfano, UPC cha Uganda na vinginevyo.
Pamoja
na hayo mrema amefafanua kwamba mahakama ya ICC haingalii tu viongozi
wa serikali bali hata viongozi wa kisiasa ambao wamesababisha mauaji
kutokana na kauli wanazozitoa.
Pia
mwenyekiti huyo wa TLP amewataka wahisani kutoingilia mambo ya ndani ya
nchi kwani kusitisha misaada kwa hoja ya kufutwa uchaguzi wa Zanzibar
na sheria ya mitandao ni kuingilia uhuru wa watanzania.