Na Lorietha Laurence-Maelezo
Jeshi
la Polisi Nchini linawashikilia watuhumiwa 14 kufuatia tukio la mauaji
ya watu watatu lililotokea katika msikiti wa Rahman eneo la Ibanda
relini mkaoni Mwanza, Mei 18 mwaka huu.
Akiongea
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Jeshi la
Polisi nchini Kamishna Msaidizi Advera Bulimba alisema kuwa msako wa
kuwakamata watuhumiwa wengine unaendelea katika maeneo mbalimbali
nchini.
Hivyo
amewaomba wananchi kutoa ushirikiano mkubwa kwa jeshi hilo ili
kufanikisha kuwakamata wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na tukio
hilo.“Nitoe wito kwa wananchi kushirikiana kikamilifu na vyombo vya
usalama katika kufichua wahalifu kwa kuwa ni watu tunaoishi nao, hivyo
hakuna budi kutoa taarifa zao ili usalama na mali zetu uendelee
kuimarika”, aliongeza Kamishna Msaidizi Bulimba.
Hata
hivyo, alieleza kuwa hali ya usalama nchini iko shwari na kuwatoa hofu
wananchi kwamba jeshi hilo limejipanga kikamilifu katika kuhakikisha
hali ya usalama inaendelea kuwepo.“Niwaombe wananchi kuondoa hofu juu ya
hali ya usalama na wasiwasi na watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola
ili kuhakikisha kwamba wote wanaojihusisha na uhalifu wanakamatwa
haraka”, alisema Kamishna Msaidizi Bulimba.
Aliongeza
kuwa uchunguzi zaidi wa matukio ya uhalifu nchini unaendelea ikiwemo
matukio ya mkoani Tanga, Dar es Salaam na mikoa mingine ili kubaini na
kuwakamata wahusika na kufikishwa katika vyombo vya sheria.Hivi karibuni
kumeripotia matukio mbalimbali ya uvunjifu wa amani katika mikoa
mbalimbali nchini ikiwemo mauaji ya watu watatu waliouawa wakiwa
msikitini jijini Mwanza.