Mke
wa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Maria Nyerere
ametembelea Daraja la Nyerere linalounganisha eneo la Kigambaoni na
Kurasini Jijini Dar es salaam na kuipongeza serikali na wananchi wote wa
Tanzania kwa kufanikisha ujenzi wa Daraja hilo kubwa na la kisasa kwa
nchi za Afrika ya Mashariki na Kati.
Mama
Maria Nyerere aliyeongozana na Mwanae Mheshimiwa Makongolo Nyerere
amesema kukamilika kwa daraja hilo ambalo ujenzi wake umegharimu
shilingi Bilioni 254.12 kumekamilisha mpango wa miaka mingi ulioanzishwa
na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa na
nia ya kujenga daraja katika eneo hilo la mkondo wa bahari lakini kwa
sababu ya ufinyu wa bajeti haikuwezekana.
Aidha,
Mama Maria Nyerere amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuamua Daraja hilo liitwe Daraja la Nyerere
kwa heshimu ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,
na amebainisha kuwa uamuzi huo utaviwezesha vizazi vijavyo kutambua
juhudi zilizofanywa na mmewe katika ujenzi wa nchi.
"Mimi
ninamshukuru sana Rais kwa maana ilikuwa lipewe jina lake, lakini yeye
Mungu akamjaalia akasema kwamba hapana tukumbuke tulikotoka, kwa hiyo
najisikia vizuri sana, na familia nayo inajisikia vizuri sana, lakini
zaidi na watanzania wanajisikia vizuri sana, kwa maana watakuwa
wanaulizana Nyerere alikuwa ni nani?" Amesisitiza Mama Maria Nyerere.
Daraja
la Nyerere lenye urefu wa meta 680, upana wa meta 3.2, njia sita za
magari na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2.5, lilifunguliwa
na Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 19 Aprili, 2016
na linakuwa kiunganishi muhimu kati ya Kigamboni na katikati ya Jiji la
Dar es salaam.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam



