Maiti ya Mariki Kimario juzi ilifukuliwa na baadaye kuzikwa upya sehemu nyingine
katika tukio jingine la kuchukua kimakosa maiti hospitalini.
Tukio kama hilo lililotokea takribani wiki mbili zilizopita kwenye Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MNH), wakati ndugu walipochukua mwili kimakosa na kwenda kuuzika
Usangi mkoani Kilimanjaro kabla ya watu wengine kupewa maiti ambayo si yao
walipoifuata hospitalini hapo na kuibua tukio hilo.
Kutokana na tukio hilo MNH ililazimika kulipa gharama za mazishi kwa familia ambayo
mwili wa ndugu yao ulizikwa na familia nyingine. Tukio hilo la juzi lilitokea mkoani Arusha
ambako Jeshi la Polisi lililazimika kusimamia kufukuliwa kwa mwili huo kwenye Kijiji cha
Elkisongo kilicho Kata ya Kidinga wilayani Arumeru.
Katika tukio hilo, ndugu walioenda
kuchukua maiti ya Leshai Ngoisaye, walipewa maiti ya Kimario na kwenda kuizika takriban
kilomita 50 kutoka Arusha mjini.
Miili hiyo ilikuwa imehifadhiwa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru. Wakizungumza na
Mwananchi jana, baadhi ya ndugu wa Kimario walisema tukio hilo limesababishwa na
kutokuwapo umakini kwa wafiwa na wahudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti.
John
Lesian, mmoja wa ndugu wa marehemu, alisema walikwenda kuchukua mwili wa ndugu
yao juzi, lakini walipofika walionyeshwa mwili wa mtu mwingine.
Hali hiyo ilisababisha kuzuka kwa malumbano baina ya ndugu wa Kimario na wahudumu
wa chumba hicho cha maiti.
“Maandalizi yote ya kuchukua mwili na kwenda kuzika Rombo yalikuwa tayari,” alisema
ndugu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jeremiah Shirima.
“Baada ya hali hii ndugu walitoa taarifa polisi na ikajulikana mwili tayari ulishachukuliwa
na kuzikwa na hivyo waliomba kwenda kuufukua.”
Muhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti wa hospitali hiyo, ambaye aliomba kutotajwa
jina, aliwalaumu ndugu wa marehemu kuwa hawakuwa makini.
“Mimi si msemaji ila tukio limetokea na tayari mwili wa Kimario umefukuliwa na
kurejeshwa na mwili wa Leshai Ngoisaye umechukuliwa na kuzikwa,” alisema
Mwenyekiti wa Kijiji cha Elkisongo alichokuwa anaishi Ngosaye, Lesiyoni Sikita alisema
tayari wamefanya mazishi mengine baada ya kuzika kimakosa mwili wa Kimario.
Mkazi wa Kijiji cha Elkisongo, Samweli Ngalabali aliomba serikali kufanya tafiti kubaini
sababu za kuongezeka kwa matukio hayo.
“Huu ni uzembe lazima serikali ichukuwe hatua,” alisema.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema ni kweli kuwa tukio hilo
limetokea na wameanza kufanya uchunguzi kujua nini kilichosababisha maiti hizo
kuchanganywa.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa Justin Urio alisema licha ya kuwa
mochwari hiyo ilibinafsishwa na sasa inafanya kazi kwa zabuni lakini uongozi wa Hospitali
nao unafanya uchunguzi kujua nini kilichotokea, hadi kupelekea maiti hizo kuchanganywa.
