Utumbuaji majipu wa Magufuli waokoa bilioni.700/-

KASI ya kuzuia ukwepaji kodi za Serikali uliofanywa kwa kipindi cha miezi mitatu na utawala wa Rais Dk. John Magufuli kwa ‘kutumbua majipu’ umeokoa wastani wa Sh bilioni 700.
Katika utawala wa Serikali iliyopita ya awamu ya nne, wastani wa makusanyo ya kodi kwa kiwango cha juu kwa mwezi yalikuwa Sh bilioni 900, lakini baada ya kuingia kwa awamu hii kumekuwapo na ongezeko la zaidi ya Sh bilioni 700 kwa miezi mitatu ya Desemba hadi Februari.
Akitangaza ongezeko hilo kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, alisema katika kipindi cha Desemba 2015, pia TRA iliweza kuvuka lengo kwa kukusanya kiasi cha zaidi ya Sh. trilioni 1.4 sawa na ongezeko la wastani wa Sh. bilioni 490 kwa mwezi.
Alisema kiasi hicho ni kikubwa kikilinganishwa na wastani wa makusanyo kwa mwezi Julai hadi Novemba mwaka jana ambapo ilikuwa ni Sh. bilioni 900 kwa mwezi.
Kidata alisema katika mkakati wa Serikali ya awamu ya tano ya Rais Magufuli ya kuhakikisha mapato ya nchi hayapotei TRA imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. trilioni 8.5 kwa kipindi cha mwezi Julai mwaka jana hadi Februari, makusanyo ambayo ni sawa na asilimia 99 ikilinganishwa na lengo la Sh. trilioni 8.6.
Kwa mujibu wa Kidata, TRA imejiwekea mikakati mizuri ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya upotevu wa mapato bandarini mwezi Februari, ambapo kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar walifanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. trilioni 1.04 ambazo ni sawa na asilimia 101.18 ya lengo la Sh. trilioni 1.02.
Alisema katika kipindi cha mwezi Januari kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar walikusanya Sh. trilioni 1.07 ambazo ni sawa na asilimia 102 ya lengo la Sh. trilioni 1.05.
Katika kipindi cha mwezi Desemba 2015, pia TRA iliweza kuvuka lengo kwa kukusanya kiasi cha zaidi ya Sh trilioni 1.4, mapato ambayo ni sawa na ongezeko la wastani wa Sh. bilioni 490 kwa mwezi ukilinganisha na wastani wa makusanyo kwa mwezi Julai hadi Novemba ambayo yalikuwa Sh. bilioni 900.
“Makusanyo hayo yametokana na uthubutu ambao TRA imejiwekea katika kusimamia na kuhakikisha inaendelea kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi na kuweka mazingira rafiki kwa mlipakodi kulipa kwa wakati na urahisi kwa kutumia mifumo mbalimbali iliyopo,” alisema Kidata.
Alisema wameweka mikakati katika ukusanyaji wa kodi kwa kipindi cha mwezi Machi hadi Juni kuhakikisha kwamba wanaendelea kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi, kufichua wakwepa kodi, kupambana na rushwa na kuongeza wigo wa kodi kwa kusajili wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa.
Pia kusimamia kwa karibu matumizi ya mashine za EFDs na utoaji wa risiti, kufuatilia na kudai malimbikizo ya kodi kutoka kwa wadaiwa sugu, kuendelea na ukaguzi wa kodi kwa wafanyabiashara ikiwa ni pamoja na maofisa wa TRA na kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu.
Katika hatua nyingine, Kidata alisema mamlaka hiyo imefuta bei elekezi kwa bidhaa zinazoingizwa nchini kutokana na kuwa ipo kinyume na sheria, huku ikilenga kutengeneza mazingira mazuri kwa wafanyabiashara ili haki itendeke katika suala zima la ulipaji wa kodi.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo