ZIKIWA zimesalia siku mbili Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumpata mrithi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, nafasi hiyo imeonekana kuwa ya moto.
Hali hiyo inatokana na kuwapo kambi kwa wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho juu ya nani anayefaa kurithi mikoba ya Dk. Slaa.
Baadhi ya wajumbe wameonekana waziwazi kupinga taarifa zilizozagaa kuwa jina la Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalim ndilo linalopewa nafasi kubwa.
Taarifa za uhakika kutoka kwa baadhi ya wajumbe na viongozi wa chama hicho, zimeeleza kuwa makundi hayo yameibuka na kuendesha kampeni za siri kila upande ukiwa na jina wanaloamini kuwa linafaa kwa ajili ya kujaza nafasi ya ukatibu.
Habari za uhakika ambazo MTANZANIA limezipata jana mjini hapa, zinasema kuna makundi matatu ambayo yanaonekana kuwa na misimamo tofauti.
Taarifa hizo, zinasema kundi la kwanza linatajwa kuwa linamuunga mkono Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye kwa madai ana sifa za kushika nafasi hiyo kutokana na uzoefu mkubwa katika masuala ya siasa.
Hata hivyo, kundi la pili limekuwa na hofu juu ya uhusiano ulipo kati ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwalimu kuwa ni moja kati ya mambo yanayoweza kumbeba na si sifa na uzoefu wake wa kutumikia nafasi hiyo nyeti ndani ya chama.
“Hii ni nafasi ambayo inahitaji mtu mzima kiasi, mwenye akili iliyotulia na ambaye anaweza kubeba mipango ya chama na majukumu yote, kama atateuliwa Mwalimu, nadhani tutakuwa bado hatujapata katibu anayekifaa zaidi chama,” alisema mmoja wa wajumbe hao.
Kwa upande wake, Mwalimu akizungumzia suala la kurithi mikoba ya Dk. Slaa, alisema huo ni uamuzi wa mwenyekiti, japo yeye binafsi hafikirii kushika nafasi hiyo kwa sasa.
“Nadhani masuala yote ya habari kazungumzeni na Tumaini Makene (Ofisa Habari wa chama), naomba sina muda kwa kuwa nipo katika maandalizi ya vikao na leo (jana) usiku tunakutana kikao cha sekretarieti…, suala la ukatibu mkuu mimi sifikirii, siwezi kujibu lolote, hili anajua mwenyekiti ambaye ndiye anapaswa kuteua,” alisema.
Habari zaidi zinasema kundi linalompigia kampeni Mwalimu limepata nguvu kutokana na taarifa za kuugua kwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Mashariki, Mabere Marando ambaye awali jina lake lilikuwa linajadiliwa mno.
“Unajua Sumaye si mzoefu, hawezi kuhimili mikikimikiki ya upinzani, hawezi, huyu alizoea siasa laini za CCM, itakuwa ngumu kukabiliana na siasa za sasa kwa kuwa hazitaki kupelekwa taratibu… kama hivyo basi, nafasi hiyo iwe ya John Mnyika,” alisema mjumbe mwingine.
Kundi la tatu nalo limekuwa likishinikiza nafasi hiyo apewe mtu anayetoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambalo limekuwa likiendesha kampeni nzito, huku likisema kufanya hivyo kutasaidia kukiondolea chama mzigo wa kuitwa chama cha Kaskazini.
“Sipingi Sumaye kuwa katibu mkuu, anafaa, lakini lazima tuangalie masilahi mapana ya chama na kuondoa ile dhana kwamba ni chama cha Kaskazini.
“Jambo hili limekuwa likitupa tabu mno, sasa kuliondoa hilo ni lazima tuwe na katibu anayetokea ukanda huu. Tunao watu wengi tu wazuri wanaoweza kushika nafasi hii, tumejiandaa kukieleza kikao cha Baraza Kuu,” alisema mmoja wa wajumbe wa mkutano huo.
Mtu mwingine anayetajwa katika nahasi hiyo, ni Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo, Benosn Kigaila.
Hata hivyo, hoja hii ilipingwa na Ofisa Habari wa chama hicho Kanda ya Ziwa Victoria, Tungaraza Njugu ambaye alisema kufanyika kwa vikao hivyo Mwanza, hakuna uhusiano na uteuzi wa katibu wala kampeni za aina hiyo.
“Kama kuna mtu ana mawazo hayo, yatakuwa yake binafsi, tuna taratibu zinazoeleweka, vikao vinakutana kwa mujibu wa Katiba… mwenyekiti anapaswa kuleta mapendekezo yake kisha yajadiliwe,” alisema Tungaraza.
Katika hatua nyingine, Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na wakurugenzi wengine waliwasili Mwanza jana usiku tayari kuanza kikao cha Sekretarieti kabla ya kikao cha Kamati Kuu inayoketi kwa siku mbili kuanzia leo.
Baada ya Mwalimu kuwasili, alifanya kikao kifupi cha kazi na waratibu wa kanda zote ambao wamefika Mwanza mapema kuendelea kusaidiana na wenyeji wa vikao ambao, ni Kanda ya Ziwa Victoria (Mwanza, Kagera na Geita) na Kanda ya Serengeti (Simiyu, Shinyanga na Mara).
Katika kikao hicho, Mwalimu alipokea taarifa fupi ya maandalizi ya awali ya vikao vya Sekretarieti, Kamati Kuu na Baraza Kuu.
Chanzo:Mtanzania