Rungu la serikali limetua Monduli...Angalia watakachofanyiwa watumishi hawa wa Serikali

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameagiza watumishi watatu wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya wilaya ya Monduli, kupandishwa kizimbani kutokana na tuhuma za wizi wa fedha za halmashauri hiyo.
Wanadaiwa kuuza viwanja zaidi ya 200 kati ya Sh milioni mbili hadi nne bila kuingiza fedha hizo katika akaunti ya halmashauri hiyo. Lukuvi alitoa agizo hilo juzi mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Francis Miti kwenye mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake wilayani humo, baada wananchi kutoa malalamiko yao ya kuuziwa viwanja hewa na watumishi wa halmashauri.
Watumishi wanaotuhumiwa ni Ofisa Ardhi Mteule wa wilaya hiyo, Kitundu Mkumbo ambaye ni Mpimaji wa ardhi , Leonard Haule pamoja na Mchora Ramani, Leonard Mkwavi. Lukuvi alisema kuwasimamisha kazi watumishi hao haitoshi hivyo ni vyema wakafikishwa mahakamani kwa kukiuka maadili ya watumishi wa umma pamoja na kurudisha fedha zote za wananchi hao waliowatapeli kwani wanalipa stakabadhi za halmashauri.
Aidha aliagiza ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kushirikiana na polisi katika wilaya hiyo, kufanya uchunguzi wa haraka na wa kina kisha kuwafikisha mahakamani watumishi hao.
Akipokea maagizo hayo, Mkuu huyo wa wilaya alisema baada ya kutambua ubadhirifu huo aliagiza watumishi hao kuwekwa ndani kwa saa 24 pamoja na kuwasimamisha kazi. Alisema uchunguzi huo umeshaanza na kwamba uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani mara moja.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) wilaya ya Monduli, Loota Sanare alimuomba waziri kufikisha ombi lao kwa Rais Dk John Magufuli kufuta hati za mashamba 39 ambayo yapo katika wilaya hiyo lakini wawekezaji wanayoyamiliki hawayaendelezi.
Akiwa wilayani humo, Lukuvi alikabidhi mashamba makubwa 13 kwa wananchi wa wilaya hiyo ambayo Rais Magufuli aliyafutia hati kutokana na wamiliki kutoyaendeleza kwa muda mrefu.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo