Mali za misitu zawatokea Puani Maafisa Misitu

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amewasimamisha kazi maofisa watano wa Idara ya Misitu mkoani Rukwa kwa kushindwa kusimamia vema na kudhibiti uvunaji haramu wa magogo.
Waliosimamishwa ni Kaimu Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Nyanda za Juu Kusini, Bruno Mallya na Mshauri wa Maliasili Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa, Nicholas Mchome kupisha uchunguzi.
Wengine waliosimamishwa kazi ni Ofisa Misitu wa TFS, Helman Ndanzi na Ofisa Misitu daraja la II, Geofrey Mwasomola wote kutoka wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa. Mwingine ni Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Sumbawanga na Kalambo, Martin Hamis.
Profesa Maghembe alisema amelazimika kuwasimamisha kazi maofisa hao kwa kushindwa kusimamia vema na kudhibiti uvunaji haramu wa magogo aina ya mkurungu na kusababisha uharibifu mkubwa katika Msitu wa Kalambo.
Pia wanadaiwa kuruhusu makundi makubwa ya mifugo kuchungwa katika msitu huo bila kuchukua hatua stahiki kwa wavamizi. Aliwaagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TFS, kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa.
“Wewe Kaimu Meneja wa TFS Kanda (Mallya ) kazi basi mpaka uchunguzi wote utakapokamilika pia Ofisa Misitu wa Mkoa wa Rukwa (Mchome) …tutaleta maofisa wengine wanaoweza kulinda rasilimali za Serikali kwa kuwa nyie mmeshindwa na hamna uchungu wa rasilimali za nchi hii,” alisema Maghembe.
Profesa Maghembe alifanya ziara jana mkoani Rukwa na kufanya kikao cha ndani na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa mkoa mjini Sumbawanga kwa zaidi ya saa mbili. Baada ya kikao hicho, Profesa Maghembe alishuhudia shehena ya magogo ya mkurungu, yaliyokamatwa na kuhifadhiwa nje ya jengo la ofisi za Mkuu wa Mkoa.
Kisha alikwenda mjini Matai ambako ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo, alikoshuhudia shehena nyingine ya magogo ya mti huo wa mkurungu yamehifadhiwa katika Kituo cha Polisi wilaya ya Kalambo tangu Desemba mwaka jana.
Pia alishuhudia lori lenye namba za usajili T427 ASG lenye kontena lililokamatwa katika kituo cha forodha Kasesya kilicho katika mpaka wa Tanzania na Zambia, likisafirisha magogo hayo kwa vibali bandia likiwa limezuiliwa katika Kituo cha Polisi wilayani Kalambo.
Vile vile alikwenda hadi katika Misitu wa Kalambo unaomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ambako alishuhudia uharibifu mkubwa uliosababishwa na uvunaji haramu wa magogo.
Magogo ya mkurungu yenye thamani zaidi ya Sh milioni 100, yalikuwa yamevunwa kinyume cha sheria. Waziri aliwapatia TFS wiki moja kuhakikisha magogo yaliyovunwa katika msitu wa Kalambo, yenye thamani ya Sh bilioni 500, yanasafirishwa na kuhifadhiwa katika kituo cha polisi. Magogo hayo sasa yamehifadhiwa katika vijiji vinne vya Kasitu, Safu Jengeni na Kaluko vinavyozunguka Msitu wa Kalambo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo