Mshtakiwa amkana Mkuu wa wilaya Mbele ya Hakimu

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hakutoa lugha chafu dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kama inavyodaiwa.

Kubenea alitoa kauli hiyo jana wakati akitoa utetezi huku akiongozwa na wakili wake, Peter Kibatala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

“Mimi sijasema hayo maneno kuwa Makonda ni mjinga, mpumbavu, kibaka na cheo chenyewe cha kupewa, bali nilimwambia wewe umeteuliwa na Rais na mimi nimechaguliwa na wananchi,” alidai.

Kubenea aliendelea kudai kuwa Desemba 14, 2015, katika kiwanda cha Tooku Garments Co. Ltd kilichopo Mabibo External kwenye mgomo wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, alimwambia Makonda hawezi kufunga mkutano bila ya yeye kuzungumza kwa sababu ni mwakilishi wa wananchi.

Alidai kuwa Makonda alimjibu kila alipokuwa akizungumza kuwa yeye ndiye mtu wa mwisho kwa kuwa ni rais wa Kinondoni. 

“Nilimjibu na mimi ni mbunge, nimeteuliwa na wananchi, lazima aheshimu uwapo wangu pale,” alidai.

Kubenea alidai kutokana na msimamo wa Makonda wa kutotaka kumpa nafasi ya kuzungumza na wafanyakazi, alimwambia hajavamia mkutano huo bali aliitwa. 

“Nikamwambia mimi siyo kibaka bali nimechaguliwa na watu, baada ya kauli hiyo, alimuamuru Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Magomeni, Denis anikamate nikapumzishwe mahabusu,” alidai.

Alidai kuwa mkuu huyo wa wilaya, aliamuru pia kukamatwa kwa raia mmoja wa China anayedaiwa kuwanyanyasa wafanyakazi hao ili achunguzwe.

Kesi hiyo itaendelea Machi 10, mwaka huu. Kubenea anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 14, 2015 katika Kiwanda hicho.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo