Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Dk. Grace Maghembe ameunda kamati kuchunguza tukio la mjamzito mkazi wa Tabata Kisiwani, Asha Sudi (17) kudaiwa
kujifungulia mtoto chooni katika Hospitali ya Amana.
“Tumepata taarifa hizo na tayari tumeanza uchunguzi wa kina
juu ya tukio hilo, tukishakamilisha tutatoa tamko,” alisema.
Juzi, Mganga Mkuu wa Amana, Dk Meshack Shimwela alikaririwa akisema hakuona
kosa kwa muuguzi kumuambia mjamzito huyo kwenda kuoga wakati akiwa na uchungu wa
kujifungua.
Mzazi huyo alisema alipofika mapokezi katika hospitali hiyo hakupimwa chochote, badala yake
aliambiwa na muuguzi aende bafuni kuoga na kubadilisha nguo.
Baadhi ya madaktari waliobobea katika uzalishaji wajawazito walisema kitendo hicho hakikuwa
sahihi kwa kuwa mjamzito anapokuwa kwenye hali ya kuumwa uchungu hapaswi kwenda kuoga
bila uangalizi wa mtalaamu wala kufanyiwa vipimo.
“Kuoga ni jambo la kawaida kwa mjamzito, lakini anapokuwa kwenye uchungu wa kujifungua
huwa hajitambui na anaweza kufanya vitu ambavyo vitahatarisha uhai wa mtoto au yeye mwenyewe,” alisema daktari ya wodi ya wazazi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita, Makoye Mayenga.
Mtaalamu wa magonjwa ya wanawake na uzazi wa Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Muhimbili, Dk
Sariel Massawe alisema mjamzito anapokuwa katika hali hiyo anatakiwa kufanyiwa vipimo ili
kujua uchungu wake uko katika hatua gani.