BAISKELI 87 na pikipiki 16 zimekabidhiwa kwa wananchi wa kata ya Kipeta na Kilangawana wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Maliasili na Utalii Jumanne Magembe.
Utekelezaji wa agizo la Waziri Magembe, limetokana na maombi ya mbunge wa Jimbo la Kwela kufuatia kilio cha wakazi wa jimbo lake kuwa wananyanyaswa na askari wa wanyamapori wa pori la akiba la Uwanda na kuwanyangíanya mali ikiwemo pikipiki na baiskeli pindi wanapopita njia kuelekea ziwa Rukwa kupata kitoweo.
Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga, Mathew Sedoyeka amewaagiza askari hao kuacha mara moja tabia ya kunyanyasa wananchi kwa madai kuwa wanatekeleza sheria kwani hakuna sheria katika nchi hii inayowaruhusu askari kumpiga raia bila kufuata utaratibu.