Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemtumia salamu za pole Mke wa
Waziri Mkuu Mstaafu Mama Tunu Pinda aliyepatwa na ajali ya gari,
iliyotokea jana tarehe 08 Februai, 2016 akiwa safarini kutoka Dodoma
kwenda Dar es salaam.
Ajali hiyo imetokea katika eneo
la Mkundi lililopo katika Manispaa ya Morogoro ambapo gari aliyokuwa
akisafiria Mama Tunu Pinda, ilipinduka baada ya kumgonga mwendesha
pikipiki aliyeingia ghafla barabarani.
Katika salamu hizo alizozituma
kupitia kwa Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda,
Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko taarifa za kutokea kwa ajali
hiyo na amemuombea Mama Pinda na Majeruhi wengine kupona haraka.
“Kupitia kwako Mheshimiwa Waziri
Mkuu Mstaafu Pinda, naomba unifikishie pole nyingi kwa mkeo Mama Pinda
kwa kuumia katika ajali hii, na namuomba Mwenyezi Mungu awaponye
majeruhi wote ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku” alisema
Rais Magufuli.
Mama Tunu Pinda anaendelea kupata matibabu Jijini Dar es salaam, na hali yake inaendelea vizuri.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
09 Februari, 2016
