Mwenyekiti akitangaza rasmi kujiuzulu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Lupalilo kata ya
Lupalilo wilayani Makete mkoani Njombe Bw. Victon Sanga amejiuzulu rasmi nafasi
hiyo jana mchana kwenye mkutano uliofanyika kijijini hapo
Hatua hiyo inatokana na sababu mbalimbali
alizozieleza katika barua yake aliyoiandika kwa na kuwasilishwa kwenye mamlaka
za kijiji hicho hivi karibuni
Katika barua hiyo iliyosomwa mbele ya wananchi
waliofika kwenye mkutano huo na kaimu afisa mtendaji wa kata hiyo Bw. Mwatima
Mbilinyi imeeleza kuwa sababu za yeye kujiuzulu ni kwenda jijini Mbeya kutafuta
maisha hali itakayosababisha kuwepo nje ya kijiji hicho kwa muda mrefu na hivyo
atashindwa kuyamudu majukumu yake ya kila siku
Amesema yeye pamoja na wajumbe wa halmashauri ya
kijiji walimshauri na kumuomba kwa muda mrefu abadilishe uamuzi wake wa
kujiuzulu lakini mwenyekiti huyo alikataa na kushikilia msimamo wake wa
kujiuzulu
Mwenyekiti aliyejiuzulu Bw. Victon Sanga amesema
pamoja na aliyoyaeleza kwenye barua ya kujiuzulu, ameongeza kuwa ameshindwa
kumudu majukumu yake ya uenyekiti kwa kuwa kila anachokifanya yeye kinaonekana
kibaya kwa wananchi
“baba wa taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema
kama unaona majukumu uliyopatiwa au kukabidhiwa huyawezi basi huna budi
kujiuzulu ili kuwapa nafasi hiyo wengine au mwingine anayeweza aifanye, sasa
mimi nimejipima nikaona niiache kwa sababu siiwezi, lakini pia ndugu zangu nao
wamenishauri kiiache na watanifadhili katika maisha mengine huko Mbeya” amesema
Bw. Sanga
Wananchi waliokuwepo kwenye mkutano huo baadhi
yao walimpongeza kwa uamuzi aliouchukua huku wengine wakisikitishwa na kitendo
chake cha kujiuzulu kwa kuwa kinakwamisha kazi za maendeleo katika kijiji hicho
“Huyu kijana tulimchagua kwa kishindo tukijua
atatusaidia lakini leo anajiuzulu, hivi sisi wana Lupalilo tutapiga hatua
kweli? Hapa kijijini kuna wazee wenye mdomo sana, naomba waache mdomo, huyu
mwenyekiti ana mengi sana moyoni hapa anaogopa kuyasema, wengine wamemtishia
kuwa tuone kama usiku utalala, hapa anaogopa kuyasema, tuache mdomo na maneno
kama hayo jamani” amesikika mwanamke mmoja akisema katika mkutano huo bila
kujitambulisha jina lake
Mwingine amesema “Huwezi kumlazimisha ng’ombe
kunywa maji sana sana utamfikisha mtoni tu, kama mwenyekiti amesoma alama za
nyakati na kuona kuwa hawezi kazi basi hatuwezi kumlazimisha”
Kutokana na nafasi hiyo kuachwa wazi ulifanyika
uchanguzi wa kumpata mwenyekiti wa kijiji atakayeongoza kwa muda hadi hapo
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete atakapoitisha uchaguzi mdogo, na Bw Method Pella akachaguliwa kuwa
mwenyekiti wa muda kwa kura 65 dhidi ya Regina Ido aliyepata kura 3
Mwenyekiti huyo ameomba ushirikiano kutoka kwa wananchi ili wafanye
maendeleo ya kijiji chao huku akikemea wale wote wenye maneno ya vitisho waache
tabia hiyo mara moja
Diwani wa kata hiyo ya Lupalilo Mh. Imani Mahenge ameahidi kutoa
ushirikiano kwa kiongozi huyo aliyechaguliwa na kuwataka wananchi kuwa na
mshikamano ili kwa pamoja wafanye shughuli za maendeleo katika kijiji chao
Mwananchi wa Lupalilo akichangia hoja ya mwenyekiti kujiuzulu
Diwani wa kata ya Lupalilo Mh Imani Mahenge akizungumza neno kufuatia kujiuzulu kwa mwenyekiti
kaimu Afisa mtendaji wa kata Bw. Mbilinyi akisema machache kufuatia uamuzi huo wa mwenyekiti
Babu Jota akichangia hoja
Wengine walisikitishwa na uamuzi wa mwenyekiti wao kujiuzulu
Wananchi wakipiga kura kumchagua mwenyekiti wa muda
Wakimpongeza mwenyekiti wa muda aliyechaguliwa
Mwenyekiti wa muda aliyechaguliwa akiwashukuru wananchi kwa kumchagua