Wahanga wa ajali ya mgodi wa dhahabu wa wachimbaji wadogo wa Nyangalata wanaotibiwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama wameuomba uongozi wa hospitali hiyo kuwapa rufaa ya kwenda hospitali ya rufaa ili kupata vipimo vya kutambua kiasi cha sumu kilichoingia mwilini wakati wakiwa wamekwama chini ya mgodi kwa siku arobaini na moja.
wametoa kilio chao kwa uongozi wa hospitali hiyo kuwawezesha kupata vipimo zaidi vya kiuchunguzi ili kujua kiasi cha sumu kilichoingia mwilini kwakuwa walitumia vyakula visivyo rasmi walipokuwa wamekwama chini ya mgodi.
Kwa upande wake mganga mkuu wa halmashauri ya mji Kahama Dr.Bruno Minja amesema uongozi wa hospitali yake umepokea ombi la wahanga hao lakini taratibu bado zinafanyika ili kuwapatia uhamisho kwenda katika hospitali ya rufaa kwa uchunguzi zaidi.
Aidha rais wa shirikisho la wachimbaji madini Tanzania "FEMATA" Bw.John Bina ameiomba serikali kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo ili kuhimili wingi wa wagonjwa wanaotoka katika maeneo ya migodi.
