Yule mgonjwa aliyeibua ubovu wa mtambo ya CT Scan na mashine ya MRI
kwa Rais John Pombe Magufuli, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini
Dar, Chacha Makenge (pichani)amekutwa na Uwazi akiwa amelala sakafuni
wodini.
Desemba 25, mwaka huu, gazeti la Uwazi ambalo ni chanzo cha habari hii lilifika hospitalini hapo Jengo la Sewa
Haji wodi namba 18 na kumshuhudia Chacha amelalia mashuka aliyoyatandika
chini huku akiwa ameshusha neti tofauti na wagonjwa wenzake waliolala
vitandani.
Chacha alisema, Desemba 24, mwaka huu, madaktari walimtaka ahame
kwenye kitanda hicho kwa sababu kuna mgonjwa mwingine alipaswa kulazwa
hapo.
“Mimi kitanda changu kilikuwa namba moja, sasa siku hiyo niliambiwa
nimpishe mgonjwa mwingine aje kitandani kwangu ndiyo nikampisha na
kuamua kulala chini kwa sababu walidai vitanda ni vichache wodini,”
alisema Chacha.
Uwazi lilimtafuta afisa habari wa hospitali hiyo, Aminiel Eligaisha
ili kumuuliza kuhusu kisa cha Chacha kulala chini wakati serikali hivi
karibuni ilinunua vitanda 300 na magodoro yake kwa thamani ya shilingi
Mil. 251 kwa ajili ya Taasisi ya Moi, lakini alisema yupo likizo na
kutoa namba za msaidizi wake, Neema Mwangomo.
Neema yeye alisema suala la Chacha kulala chini au kinyume chake
linahusiana na uongozi wa Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi).
Alipopigiwa msemaji wa Moi, Almasi Jumaa simu yake haikupatikana hewani.
Novemba 9, mwaka huu, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza
kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moi ambapo alipata
maelezo kutoka kwa uongozi sambamba na baadhi ya wagonjwa kumweleza kero
yao.
Miongoni mwa wagonjwa hao ni Chacha ambaye alimwambia rais kuhusu
ubovu wa mashine za CT-Scan na MRI akisema kuharibika kwake ndiko
kunamfanya yeye aendelee kulazwa hapo kusubiri zipone na kufanyiwa
vipimo. Rais aliagiza mashine hizo zitengenezwa haraka sana
Chanzo:Uwazi