Baba mzazi wa watoto wawili, Lucas Petro mwenye umri wa miaka
29, anatafutwa na polisi kwa kosa la kuwachoma moto watoto wake, Denis
(5) na Ester Lucas, 3, (pichani) baada ya kuwatuhumu kuiba mboga aina ya
samaki kwa jirani yao, tukio lililotokea katika Kijiji cha Msasa, Kata
ya Busanda wilayani Geita, mwishoni mwa mwezi Novemba, mwaka huu.
Wakizungumza katika ofisi za mtendaji wa kata kijijini hapo, watoto
hao ambao wameunguzwa mikononi, miguuni na midomoni, walisema
walifanyiwa vitendo hivyo baada ya baba yao kuwafungia majani kabla ya
kuwachoma moto, kwa kitendo chao cha kula mboga yote ya jirani yao,
Maneno Balinozya.
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Hamis Mandikilo alidai kuwa watoto
hao waligunduliwa Desemba 12, mwaka huu majira ya saa 6 mchana wakati
wajumbe wa kamati ya huduma ya jamii walipokuwa wakipita kila kaya
kuhamasisha zoezi la usafi wa mazingira.
Alisema baada ya kuwagundua, waliwachukua hadi ofisini kwake na
kuamuru mgambo wamkamate baba yao kwa hatua zaidi za kisheria, ambapo
walifanya hivyo na kumfikisha ofisini kwake kwa mahojiano zaidi kabla ya
kumpeleka polisi.
“Walipomfikisha ofisini kwangu nilimhoji na alikiri kutenda kosa hilo
kwa madai kuwa watoto hao walikwenda kwa jirani yao Balinozya na
kukomba mboga na ndipo alipoamua kuwafungia majani makavu kisha
kuwalipua moto,’’ alisema.
Kufuatia hali hiyo, mtendaji huyo aliamua kumfikisha mtuhumiwa huyo
ofisi ya mtendaji wa kata hiyo, Juster Mabala ambako alishikiliwa kwa
siku mbili mfululizo hadi alipowatoroka walinzi wa ofisi hiyo na
kutokomea kusikojulikana.
Wakati polisi wakiendelea kumsaka, watoto hao wanatibiwa katika
hospitali ya wilaya kwa gharama za ofisi ya mtendaji wa kata hiyo.