Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufikia Desemba 9 mwaka huu ambapo ni maadhimisho ya Uhuru itakayoadhimishwa kwa kufanya usafi nchi nzima, wilaya ya Makete mkoani Njombe imezidi kutilia mkazo agizo hilo la Rais
Akizungumza wakati akitoa taarifa kwenye baraza la madiwani Makete, afisa afya wa wilaya Bw. Boniphace Sanga amesema wilaya ya Makete kwa mwaka jana ilishika nafasi ya pili kitaifa kwa usafi wa mazingira hivyo kuwaomba madiwani kuipokea kampeni hiyo na kwenda kuitilia mkazo kwa vitendo kwenye kata wanazotoka
"Tunachokitafuta mwaka huu ni kushika namba moja, na ninaimani tunaweza, ninawaomba waheshimiwa madiwani kila mmoja akahamasishe huko atokako ili tushike namba moja kwa usafi wa mazingira na inawezekani kwani hapa kazi tu" amesema Sanga
Desemba 9 mwaka huu maadhimisho ya uhuru yataadhimishwa kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchi nzima kwa agizo la Rais Magufuli aliloagiza usafi ufanyike nchi nzima ili kupambana na ugonjwa wa kipindupindu ambao umeshika kasi katika maeneo mbalimbali hapa nchini