Wanajeshi wastaafu zaidi ya 4000 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania mkoa wa Morogoro wamelalamikia serikali za awamu zilizopita kuwatelekeza bila kuwahudumia.
Wanajeshi wastaafu zaidi ya 4000 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania mkoa wa Morogoro wamelalamikia serikali za awamu zilizopita kuwatelekeza bila kuwahudumia ingawa walistaafu wakiwa na taaluma mbalimbali hivyo wameiomba serikali ya awamu ya tano kuwatazama kwa jicho la tatu ili waondokane na hali ngumu ya maisha inayowakabili.
Akizungumza mjini Morogoro kwenye kikao cha Muungano wa Wanajeshi Wastaafu Tanzania (MUWAWATA) mwenyekiti wa muungano huo Sajent Taji mstaafu Asseidy Mayuggi amesema Tanzania inashindwa kuendelea kiuchumi kutokana na serikali kutumia wataalamu wa nje huku wakiwa na hazina ya wanajeshi wastaafu wenye uwezo wa kushiriki katika kufanya kazi na kuchangia pato la taifa.
Wamemuomba amiri jeshi mkuu Rais wa awamu ya tano Dkt John Magufuli kutumia mamlaka aliyonayo kuwatumia wastaafu hao.
Kwa upande wao wajane wa wanajeshi waliofariki wakiwa kazini wamelalamikia jeshi hilo kusitisha malipo ya kujikimu pamoja na kuwasomesha yatima walioachwa na wazazi wao ambapo wamesema wameshindwa kuwaendeleza kimasomo kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili.
Katika kuhakikisha wastaafu wanaepuka kuishi maisha ya utegemezi mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii (NSSF) umeendelea kusajili wanajeshi wastaafu wajiunge na mfuko huo kwa lengo la kupatiwa huduma za matibabu bure, kupata mkopo wenye riba nafuu pamoja na mitaji itakayowawezesha kuendesha maisha kuliko kuendelea kuilalamikia serikali.