Mtu mmoja aliyekuwa akituhumiwa kumuua mwenzake kwa kumtenganisha kichwa na kiwiliwili, amehukumiwa kunyngwa hadi kufa.
Mkazi wa Kidete wilayani Kilombero mkoani Morogoro Ayoub Mangungu (39) , aliyekuwa akikabiliwa shitaka la kumuua kwa kumtenganisha kichwa na kiwiliwili mwenzake na kumfukia kwenye shimo mwenzake, amehukumiwa kunyongwa hadi kufa na mahakama kuu kanda ya Dar es salaam.
Mshitakiwa huyo aliyekuwa akitetewa na wakili Ignas Punge, amepatikana na hatia ya mauaji ya kukusudia na kupewa adhabu hiyo ya kunyongwa hadi kufa na jaji wa mahakama kuu kanda ya Dar es salaam, Eliezer Feleshi, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na kwa kuzingatia kuwa mshtakiwa amekiri kutenda kosa hilo.
Awali imedaiwa na wakili wa serikali Glory Rwakibalila kuwa mshtakiwa ametenda kosa hilo Julai 22, mwaka 2011, majira ya saa 3 usiku, huko kijiji cha Kidete, ambapo amemuua kwà kumtumbukiza mtoni, Deogratius Mwafongo na kumkata shingo kwa kutumia mundu na jembe na kumfukia kwenye shimo shambani.