Watu wanne akiwemo askari Polisi, mkaguzi na wasimamizi wa mitihani ya kidato cha nne Arusha wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kukutwa wakivujisha mtihani wa Kiswahili uliokuwa unatarajiwa kufanyika Novemba 20 mwaka huu.
Mtihani huo ulijulikana kuwa umesambaa katika shule ya Sekondari Arusha baada ya wanafunzi kugawiwa na wakati wanausoma ndipo walipogundua kuwa si wa Novemba 2 kama ulivyopangwa bali ni wa Novemba 20 ndipo walipoamua kutoa taarifa wasimamizi.
Mkurugenzi wa jiji la Arusha Idi Juma alisema mtihani huo ni wa watahiniwa wa kujitegemea ambao hufanya mitihani miwili na watu hao walijichangaya badala ya kuchukua mtihani wa Kiswahili wa awamu ya kwanza walichukua wa awamu ya pili.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo hakuweza kuwataja majina wahusika kwa madai kuwa bado wanaendelea na upelelezi kubaini chanzo cha tukio hilo.