Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli amefuta safari zote za nje ya nchi kuanzia leo hadi hapo maamuzi mengine yatakapotolewa.
Dk Magufuli ameagiza shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje.
Uamuzi huo wa rais ameutoa Ikulu jijini Dar es Salaam katika kikao kilichojumuisha watendaji mbalimbali wa serikali wakiwemo Makatibu wakuu, Manaibu Makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari ruhusa ya safari nje ya nchi inaweza kutolewa kwa jambo la dharura ambalo hata hivyo jambo hilo lazima lipate kibali cha Katibu Mkuu Kiongozi.
Katika kikao hicho, rais ameelekeza pia mambo kadhaa ambayo watendaji hao wanapaswa kuyasimamia, kuyawekea mikakati na kuyapanga vizuri ili yasimamiwe mara moja na Baraza la Mawaziri atakaloliteua.
Mambo hayo ni pamoja na kuanza kwa mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wote wanaanza kupatiwa elimu ya bure kuanzia Januari mwakani.
Taarifa hiyo imetaja jambo la pili kuwa ni suala la uratibu wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ambapo ameagiza lifanyiwe kazi na mipango yake ikamilike kwa ajili ya utekelezaji mzuri zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, rais amemuagiza Kamishna wa TRA kusimamia kwa makini zoezi la ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kero ndogo ndogo zinazowakabili wananchi zinaanza kushughulikiwa mara moja.
Ameitaka TRA kukusanya mapato toka kwa wafanya biashara wakubwa na wakwepa kodi bila kuogopa mtu wala taasisi yoyote na kusisitiza kuwa hakuna mwenye mamlaka ya kubatilisha maamuzi hayo zaidi yake.
Dk Magufuli ametaka usimamizi mzuri katika suala la manunuzi ya umma ambalo amesema limekuwa likitumika vibaya na kuwa mwanya wa maofisa wasio waaminifu kuiibia serikali kwa kuongeza bei za bidhaa na huduma tofauti na bei halisi ya manunuzi.