Dkt. Magufuli Aapishwa Rasmi Kuwa Rais wa Jamhuri Ya Muungano Tanzania


Hatimaye, Dkt. John Magufuli ameapishwa rasmi na kuwa Rais wa serikali ya awamu ya Tano ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania akihitimisha rasmi uongozi wa serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
 
Rais Magufuli na makamu wake Bi. Samia Suluhu wamekula kiapo leo katika sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam mbele ya viongozi wa nchi mbalimbali pamoja na viongozi wa chama, serikali na viongozi wa dini ambazo zilinogeshwa zaidi na gwaride la Jeshi la Wananchi.
 
Dkt. Magufuli ameapishwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Othman Chande na kupigiwa mizinga 21 ya heshima baada ya kukabidhiwa kijiti cha uongozi na rais wa serikali ya awamu ya nne, Jakaya Kikwete.
 
Katika Jukwaa la Kiapo, walikuwepo Jaji Mkuu, Othman Chande, Katibu Mkuu Balozi Ombeni Sefue pamoja na Spika wa Bunge la 10, Bi. Anne Makinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
 
Wengine waliokuwa katika jukwaa la Kiapo ni pamoja na Rais wa serikali ya awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais wa serikali ya awamu ya nne, Dkt. Gharib Ali Bilal, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Ali Shein.
 
Rais wa awamu ya nne, alipigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride maalum la jeshi la Wananchi kama  ishara ya kumuaga kwa heshima na kuteremsha bendera yake, kabla hajakabidhi madaraka kwa rais mpya Dkt. Magufuli.
 
Pia, viongozi wa dini za aina Tatu walihusika katika kuunda jopo la kiapo na kutoa sala zao kuliombea Taifa na Rais Mpya, Dkt. John Magufuli.
 
Marais wa nchi mbalimbali waliohudhuria ni pamoja na Paul Kagame (Rwanda), Jacob Zuma (Afrika Kusini), Robert Mugabe (Zimbabwe), Uhuru Kenyatta (Kenya), Yoel Museven (Uganda), Rais wa Msumbiji pamoja na mawaziri wa nchi mbalimbali.
 
Sherehe hizo zilihudhuriwa na maelfu ya wananchi na kupata baraka ya mvua wakati wote lakini wananchi hao waliendelea kufuatilia tukio hilo la kihistoria.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo