MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Arusha Mjini, God Mwalusamba amewataka wakazi wa Jiji la Arusha kutomchagua mgombea ubunge wa Chadema, Godbless Lema, kwani endapo atapewa fursa ya kwenda bungeni huenda akaishia kususa vikao badala ya kupigania maendeleo ya Wana-Arusha.
Mwalusamba alisema mbali ya kususa vikao vya Bunge na kutoka nje, hiyo itakuwa pigo katika Jimbo la Arusha Mjini kwani maendeleo ya jiji hilo yatakuwa ndoto kama miaka mingine aliyokuwa madarakani.
Alisema maamuzi sahihi yanayoendana na kasi ya Rais John Magufuli kwa kumchagua mbunge atakayefanya kazi na kiongozi huyo wa nchi na siyo atakayemkwamisha kwa kususia vikao na kutoka nje ya Bunge.
Alisema hayo juzi katika uzinduzi wa kampeni za ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa upande wa CCM na kuwataka wananchi hao kumchagua mgombea wa CCM, Philemon Mollel ` Monaban’.
Alisema wananchi wa Arusha Mjini hawana haja ya kusubiri kuambiwa nini cha kufanya, bali wanapaswa kufanya maamuzi hayo sahihi ya kumchagua Monaban kwa kuwa juzi walijionea wenyewe kwa macho yao jinsi wabunge wa Ukawa walivyofanya vituko wakati Rais Magufuli alipokwenda kwa ajili ya kulihutubia Bunge.