Watoto wawili wenye umri wa miaka 13
wamebakwa kwa nyakati tofauti, huku mmoja akidaiwa
kufanyiwa ukatili huo na baba yake wa kambo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda
alisema tukio hilo lilitokea eneo la Mtaa wa Kashai alfajiri ya Novemba 15 mwaka huu.
Alidai kuwa siku ya tukio, mtuhumiwa alitoka chumbani kwake alikokuwa amelala na mkewe na
kwenda chumba alichokuwa amelala binti huyo ambaye alimwamsha na kumpeleka kwenye
pagala lililokuwa jirani na nyumba yao ambako alimbaka.
“Kutokana na maumivu, mtoto huyo
alipiga kelele, mama yake na majirani walimsikia wakatoka na kumkuta mtuhumiwa akiendelea
kufanya kitendo hicho,” alidai.
Alisema polisi wanamshikilia mtuhumiwa kwa uchunguzi kabla ya kumfikisha mahakamani mara
watakapoukamilisha.
Katika tukio lingine, polisi wanamsaka mwendesha bajaji mmoja anayedaiwa kumbaka binti
mwingine wa miaka 13.
Kamanda Mwaruanda alisema binti huyo alifanyiwa kitendo hicho Novemba 18, saa 10 jioni
baada ya kukodi bajaji hiyo kutokea Soko la Mandela ili impeleke mtaa wa Edeni B.
Alidai kuwa wakiwa njiani, ghafla dereva huyo alibadili njia na kumpeleka kwenye kichaka
kilicho karibu na Kanisa la Hija.
“Huko alimbaka na kumtelekeza hapo kabla ya kutokomea kusikojulikana,” alidai Kamanda
huyo.
Alisema tayari watoto hao wameshapatiwa matibabu Hospitali ya Mkoa Sumbawanga na hali
zao zinaendelea vizuri.
“Bado tunaendelea kumsaka mtuhumiwa mara tutakapomtia mbaroni tutamfikisha
mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake ili kukomesha vitendo hivi,” alisema.