Baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa ubunge jimbo la Makete mkoani Njombe, chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA wilayani humo kimezungumza kwa mara ya kwanza baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu
Akizungumza wakati akihojiwa katika kipindi cha Morning Alarm kinachorushwa na kituo cha redio Green Fm cha mkoani Njombe, aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Makete Jackson Taifa Mbogela amesema uchaguzi umemalizika na wamekubali kuwa wameshindwa katika uchaguzi huo na kwa sasa wanajipanga katika uchaguzi mkuu ujao
Mbogela amesema wanajipanga kwa uchaguzi mkuu ujao na anaimani kuwa upo uwezekano mkubwa wa kushinda kutokana na kura zaidi ya elfu 15 alizopata katika uchaguzi wa mwaka huu
"Ninawashukuru sana wananchi wa Makete kwa kukiamini chama cha CHADEMA na kutupatia kura zaidi ya elfu 15, na kizuri zaidi tumepata madiwani 7 kitu ambacho hakijawahi kutokea Makete, hatuna budi kuwashukuru sana wananchi" amesema Mbogela
Amesema wakati akiwa kwenye kampeni waligundua changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya miundombinu hasa barabara kuwa mbaya jambo linalopelekea kero kubwa kwa wananchi wa vijiji mbalimbali vya wilaya ya Makete vinavyotegemea barabara hizo kwa ajili ya shughuli zao za kimaendeleo
Aidha amemtakia kila la heri mbunge aliyechaguliwa kupitia chama cha mapinduzi CCM Prof Norman Sigalla King, kuhakikisha anatekeleza ahadi zake alizowaahidi wananchi kwa kuwa ndicho wanachokihitaji
Mtangazaji wa Green Fm Henrick Idawa akifanya mahojiano na aliyekuwa mgombea ubunge makete kupitia CHADEMA Jackson Mbogela
Jackson Mbogela akijibu hoja za wasikilizaji wa Green FM
Akiendelea kuwashukuru wananchi wa jimbo la Makete
Picha na Edwin Moshi