Hatimaye Chama cha ACTWazalendo mkoani Arusha
kimempata mgombea atakayepeperusha bendera yake katika
uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini.
Hatua hiyo imekuja baada ya chama hicho kuhaha kwa siku
kadhaa hadi dakika za mwisho kumpata mtu wa kuwania jimbo
hilo baada ya uchaguzi kuahirishwa kutokana na kifo cha
aliyekuwa mgombea kupitia chama hicho, Estomih Mallah
kufariki dunia katikati ya kampeni.
Katibu wa chama hicho mkoani Arusha, Daniel Olotu alimtaja
Navoy Mollel kuwa ndiye mgombea atakayepeperusha bendera
ya chama hicho baada ya kushinda katika kura za maoni kwa
kupata alama 62.
Olotu alisema mkutano mkuu wa chama hicho ulimpitisha Mollel baada ya kuwashinda wenzake
wanane, akifuatiwa na Hagai Mollel aliyepata kura 34 na John Saitabau aliyepata kura 22.
Uchaguzi huo unafanyika sambamba na majimbo mengine matatu ya Ulanga Mashariki, Handeni
Mjini na Ludewa ambako wagombea wa CCM walifariki dunia pamoja na Lushoto ambako
mgombea wa Chadema alifariki dunia.