Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro,
imewahukumu watu wawili kutumikia kifungo cha miaka 15 jela
kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila ya
kukusudia Nasrah Mvungi maarufu kama ‘mtoto wa boksi’
wakati akiwa na umri wa miaka minne.
Jaji Elieza Mbuki alitoa hukumu hiyo jana baada ya kuwatia
hatiani washtakiwa hao Mariamu Said (39) na mumewe Omar Mtonga kutokana na ushahidi ulitolewa mahakamani hapo
kuthibitisha bila kuacha shaka kuwa walitenda kosa hilo.
Jaji Mbuki alisema mahakama hiyo imeridhishwa na ushahidi huo uliotolewa na upande wa mashtaka na kuwatia hatiani washtakiwa hao kisha kuwahukumu kifungo hicho jela ili iwe
fundisho kwao na kwa watu wengine wenye tabia kama zao.
Washtakiwa hao na baba wa mtoto huyo, Rashid Mvungi walifikishwa mahakamani kwa mara ya
kwanza na kusomewa mashtaka ya kula njama na kufanya vitendo vya kikatili dhidi ya Nasrah.
Mwanasheria wa Serikali, Janeth Kisibo alidai washtakiwa hao, walitenda makosa hayo Desemba
2010 na Mei 2014 na kuathiri afya ya mtoto huyo.
Alidai shitaka hilo lilibadilika kuwa la mauaji baada ya Nasrah kufariki Juni Mosi, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikolazwa kwa matibabu.
Wakati kesi hiyo ikiendelea, mshtakiwa wa tatu aliachiwa huru.