Wanaume kadhaa wa eneo la Sirari, jana walishindana
kupiga ‘pushapu’ mbele ya mgombea mwenza wa urais wa CCM,
Samia Suluhu Hassan baada ya kuvutiwa na sera zake.
Hatua ya wanaume hao ilisababisha kuvuma kwa kelele za
shangwe katika uwanja wa Tarafa, mahali mkutano wa kampeni wa mgombea huyo ulipofanyika.
Kabla ya ‘pushapu’ hizo ambazo zimepachikwa jina la Magufulika, Samia alinadi Ilani ya CCM
akisema imejipanga kuwawezesha wananchi kupiga hatua mbele kiuchumi.
Alisema pamoja na kukusudia kujenga viwanda, pia wanakusudia kuboresha maeneo yenye fursa
za kibiashara.
“Tunajua Soko la Remangwe bado linajengwa, tutahakikisha tunalikamilisha ili kutanua fursa za
kibiashara kwa Sirari na Mkoa wa Mara kwa ujumla,” alisema Samia.
Pia, alisema wamepanga watakapofanikiwa kuingia madarakani kuanzisha mamlaka ya biashara
ndogo itakayosimamia shughuli kama vile za mama lishe na waendesha bodaboda.
“Tunataka wajiunge katika vikundi ili waweze kupata mikopo itakayotolewa kwa udhamini maalumu wa Serikali, hivyo itasaidia kukuza mitaji na biashara zao kwa ujumla,” alisema.
Samia alisema wanakusudia kuwatengea wafanyabiashara hao maeneo maalumu ya kufanyia
shughuli zao ili kuwaepusha na kero ya askari mgambo.
Mgombea huyo mwenza alisema wamepanga kuwajengea waendesha bodaboda mazingira mazuri
ya kazi, kwa kutenga vijiwe kwenye kila kituo na kuviwekea rangi maalumu kudhibiti vitendo vya
uhalifu vinavyofanywa, hasa maeneo ya mjini.
