Kada wa CCM anayetetea ubunge wa Peramiho,
Jenista Mhagama amewataka wapiga kura wake kupuuza sera
za wapinzani wanaopita jimboni humo na kuwaporomoshea
matusi wagombea wa chama hicho.
Badala yake, amewataka wawajibu Oktoba 25 kwa kuwachagua
wagombea wa CCM ili waendelee kuwaletea maendeleo.
Jenista alisema hayo jana katika kampeni zake alizofanya katika
Kata ya Matimila.
Aliwataka wanachama na wakazi jimboni humo kutojibu matusi hayo ili
kuepusha shari.
“Nafurahi katika kipindi chote cha uongozi wangu nimeboresha maisha ya wananchi kwa kutatua
kero kama nilivyowaahidi kwa asilimia 95,” alisema.
Alizitaja baadhi ya kero hizo kuwa ni za maji, ujenzi wa barabara, umeme na kuanzisha miradi ya
vikundi vya vijana na wanawake jimboni humo.
Awali, akifungua mkutano huo wa kampeni, Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, Rajab
Uhonde, aliwataka wananchi kumchagua Jenista ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya WaziriMkuu, Sera, Uratibu na Bunge kuwa mbunge wao tena kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
“Nawapongeza kwa kuendelea kuwa na imani na Jenista, ndiyo maana hata kwenye chama
hakuwa na mpinzani. Nawaomba mumpigie kura nyingi pamoja na mgombea urais wa CCM, Dk
John Magufuli na wagombea udiwani wote wa CCM,” alisema Uhonde.
Mkazi wa Kata ya Matimila, Maria Nyoni alimpongeza Jenista kwa kugawa mitaji kwa vikundi vya
wanawake na vijana ili waweze kujikwamua na umaskini.
Alisema katika kipindi chake cha ubunge, alikuwa akitatua kero za wakazi wa jimbo hilo bila
upendeleo.