Wanaodaiwa kuchoma ofisi ya Serikali wafikishwa kwa pilato

Watuhumiwa 14 kati ya 106 waliokamatwa na Polisi mjini Moshi juzi kwa tuhuma za kuchoma ofisi ya Serikali ya kata jana walipandishwa kizimbani kujibu tuhuma hizo. 

Washukiwa wengine 92 ambao nao walifikishwa eneo la mahakama jana asubuhi sambamba na washitakiwa hao 14, walirudishwa kituo cha kati cha polisi ili waweze kudhaminiwa. 

Watuhumiwa hao walirejeshwa polisi ili wadhaminiwe wakati polisi ikiendelea na uchunguzi ikiwamo kuwachuja wale wanaodaiwa kuhusika moja kwa moja na tukio hilo. 

Ofisi hiyo ilichomwa moto na kundi la wananchi waliokuwa wakipinga ushindi wa Jomba Koyi wa Chadema, aliyetangazwa kuwa mshindi wa kiti cha udiwani cha kata hiyo ya Njoro. Eneo la mahakama ya wilaya ya Moshi, lilifurika ndugu, jamaa na marafiki wa watuhumiwa hao wakiwamo makada wa CCM walijitokeza kwa lengo la kuwadhamini. 

Aliyekuwa kivutio mahakamani hapo ni aliyekuwa mgombea Ubunge Jimbo la Moshi mjini kwa tiketi ya CCM, Davis Mosha ambaye alishangiliwa kwa nguvu na watuhumiwa waliokuwa mahabusu. 

Waliofikishwa mahakamani hapo ni Bakari Ally(41), Ally Mkunda(34), Azama Ramadhan(35), Idd Hussein (26), Aisha Ramadhan (23), Amina Bakari (55), Mohamed Ally(62) na Miraji Ramadhan(32). Wengine ni Pazima Lema (27), Amir Juma (27), Freeman Ebati (25), Justine Shemweta (34), Alli Hassan(32) na Msafiri Yona (29) huku eneo lote la mahakama likifurika ndugu, jamaa na marafiki. 

Washitakiwa hao walisikika wakiimba “Jembe, Jembe, Jembe” wakati Mosha alipofika mahakamani hapo kuwafuatilia washitakiwa hao na baadae kupanda ngazi kuelekea vyumba vya mahakama. 

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa mahakamani hapo na mawakili wa Serikali, Baraka Nyambita na Omary Kibwana, washitakiwa hao 14 walishitakiwa kwa makosa mawili ya Jinai. 

Mbele ya Hakimu wa wilaya ya Moshi mfawidhi, Joachim Mwilapo, mawakili hao walidai kuwa Oktoba 28 mwaka huu, walifanya mkusanyiko usio halali ambao ulipelekea uvunjifu wa amani. Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku hiyo hiyo, washitakiwa walifanya uharibifu wa mali za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizokuwa katika ofisi hiyo ya kata ya Njoro. Vitu vilivyoharibiwa katika tukio hilo ni pamoja na meza saba, viti vya plastic 13, viti vya mbao 7, makabati ya ofisini mawili na fedha taslim sh110,000 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Washitakiwa wote walikana mashitaka hayo na kudhaminiwa kwa masharti ya kuwa na mdhamini atakayesaini hati ya dhamana ya Sh1 milioni. 

Washitakiwa wote walitimiza masharti hayo. Upande wa mashitaka ukiongozwa na mawakili Nyambita na Kibwana, uliiambia mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na Novemba 17 usikilizwaji wa awali umepangwa kuanza. 

Katika tukio lingine, jana watu wasiofahamika walifanya jaribio la kuchoma ofisi ya CCM kata ya Bomambuzi katika Manispaa hiyo, kwa kuimwagia kimiminika kinachoaminika ni mafuta ya Diesel. 

Hata hivyo, mlinzi wa ofisi hiyo alifanikiwa kuudhibiti moto huo ambao uliunguza baadhi ya nyaraka za ofisi hiyo, ikiwa ni siku chache tu baada mgombea wa Chadema kushinda kiti cha udiwani. 

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia jana na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi kuwabaini wahusika.  


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo