Chama cha walimu (CWT) Wilaya ya Makete mkoani Njombe kimeitaka serikali kuwalipa madeni ya walimu ya zaidi ya shilingi milioni 300 wanayoidai
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CWT wilaya ya Makete Mwl. Thobias Kasambala (pichani) wakati akitoa tamko lao la kuunga mkono kauli ya rais wa chama hicho taifa Gratian Mkoba katika kipindi maalum kilichorushwa moja kwa moja na kituo cha Redio Green Fm wilayani hapo jana usiku
Amesema madai yao yanatokana na masuala mbalimbali ikiwemo mishahara, fedha za masomo, fedha za kuhama, walimu wastaafu, na walimu waliostaafu kwa hiari
Amedai kuwa madai yao hayalengi kuikomoa serikali na wamelazimika kuyatoa kipindi hiki kwa kuwa hivi karibuni katibu mkuu wa Utumishi alisikika akiutangazia umma kuwa walimu hawaidai serikali jambo walilosema si kweli
"Ndugu mtangazaji hivi karibuni katibu mkuu Utumishi alisikika akisema walimu hawaidai serikali, ni kweli serikali inalipa madeni ya walimu, lakini bado inadaiwa, sasa kitendo na serikali kusema haidaiwi na wakati sisi wa makete ni miongoni mwa walimu tunaoidai serikali hii si sawa kabisa, na ndio maana tumeona tuutangazie umma kuwa tunaidai serikali" amesema Mwalimu Thobias
kasambala ametoa wito kwa walimu wote wilayani Makete kuendelea kufundisha na kutekeleza majukumu yaoa kama kawaida licha ya kuidai serikali, kwa kuwa wanaimani serikali itawasikia na itafanya nao mazungumzo ambapo wamesema hadi kufikia Januari 2016 kama madai yao yatakuwa hayajatekelezwa watalazimika kwenda kwenye hatua nyingine ya namna ya kudai ambayo hakuitaja ni ipi