WASHITAKIWA nane wamefikishwa mahakani kwa kosa la jinai ya kukusanya matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Urais mwaka huu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuyachapisha kupitia mitandao ya kijamii bila ya kuihusisha tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Washitakiwa hao, Mashinda Edwin Mtei (45),Mkazi wa Tengeru-Arusha, Julius Mwita (30), Mkazi wa Magomeni-Dar es Salaam, Frederick Eddie Fussi (25), Mkazi wa Mbezi beach-Dar es Salaam, Meshack Carlos Mlawa (27), Mkazi wa Keko-Dar es Salaam, Anisa Nicholas Rulanyaga (41), Mkazi wa Kawe-Dar es Salaam, Jose Mavinga Nimi(51), Mkazi wa Paris-Ufaransa, Julius Mwonga Matei (45), Mkazi wa Mwangazi-Kitui, Kenya na Kim Hyunwook (42) wa Busan-Korea Kusini.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa tukio hilo litokea kati ya Oktoba 25 na 26 mwaka huu katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam, kupitia mtandao wa kitaifa wa usimamizi wa uchaguzi uliopewa jina la “Mfumo wa usimamizi wa matokeo ya uchaguzi wa M4C” (M4C National Results management system) na mitandao mengine ya kijamii ya Facebook na Twitter.
Mahakama ya Kisutu imesikiliza kesi hiyo mbele ya hakimu mkazi kisutu, Respicius Mwijage baada ya kufahamika kuwa data za watuhumiwa hao zilizowekwa mitandaoni hazikuwa sahihi na hazikuwa na ukweli wowote, yanayodaiwa kupotosha umma juu ya matokeo yanayoendelea kutolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Makosa mengine kwa washitakiwa no.4, 7 na 8, ambao ni Julius Mwonga Matei, Jose Mavinga Nimi na Kim Hyunwook wanatuhumiwa kujihusisha na ajira bila kibali siku ya Oktoba 26 wakiwa katika hotel ya King D iliyopo wilaya ya kinondoni wakiwa na vitambulisho vya uraia wa Kenya, Angora na Korea, vyenye No. A.1532119, 30879 na M.27687807 wakishiriki katika ajira ya kukusanya na kuchapisha matokeo ya uchaguzi wa Rais kwa CHADEMA bila ya uhalali wa kibali.
Mahakama inawashitaki kwa tukio hilo lililodaiwa kwenda kinyume na kifungu cha 16(1) na 31(1)(m) cha sheria ya uhamiaji ya mwaka 2002 ambayo ni sawa na Sheria No.8 iliyofanyiwa marekebisho mwaka huu.
Kosa lingine la mshitakiwa no.4, Julius Mwonga, ni kujihusisha katika biashara kwa niaba ya WANAMA SACCOS bila ya kibali akiwa na kitambulisho chake cha uraia wa Kenya chenye No.A.1532119.
Mshitakiwa anashitakiwa kwa kwenda kinyume na kifungu cha 16(2) na 31(1) cha sheria ya uhamiaji ya mwaka 2002 ambayo ni sawa na Sheria No.8 iliyofanyiwa marekebisho mwaka huu.
Mahakama imetoa tarehe ya kuamua kutoa au kutotoa dhamana kwa watuhumiwa hao hadi Oktoba 30 mwaka huu, ambapo kwa upande wa watuhumiwa kesi hiyo inasimamiwa na mawakili wawili, Peter Kibatala na Omary Msemo ambao wamempinga mwanasheria wa Serikali dhidi ya kuitaka mahakama itoe dhamana kwa watuhumiwa hao.
Hoja za mawakili hao wawili ni mbili ambazo zinahoji juu ya Maslahi ya Umma yaliyoelezwa katika kesi hiyo ni yapi huku wakiitaka hoja ya uholela inayozungumzwa katika kesi hiyo ifafanuliwe.
Mbowe akiagana na vijana hao baada ya kunyimwa dhamana