Mamlaka ya Chakula na Dawa Kanda ya Ziwa (TFDA), imeteketeza pombe ya viroba ‘feki’ aina ya empire, signature vodka na bidhaa nyingine zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 83 zilizokutwa zimetengenezwa katika kiwanda cha Simba Gin cha jijini Mwanza.
Mkuu wa ukaguzi wa mamlaka hiyo mkoa wa Mwanza, Julius Timothy, alisema pombe hizo zilizoteketezwa zilikuwa tani 15.18 na zilikuwa zimefichwa katika kiwanda hicho, lakini wasamaria wema walitoa taarifa na kufanikiwa kuzikamata.
Timothy alisema wamiliki wa kiwanda hicho waliamua kutumia nembo ya vinywaji hivyo vinavyotengenezwa nchini Uganda ili kuwaaminisha wanywaji ni bidhaa halali kwa matumizi huku wakifahamu ni kinyume na sheria.
Baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi, tulifika katika kiwanda hicho ambako tulikuta bidhaa mbalimbali ikiwamo pombe aina ya empire na signature vodka, tulifanikiwa kuzikamata, kitu kibaya wanatumia nembo ya vinywaji halali toka Uganda,îalisema Timothy.
Alisema kiwanda hicho kimefungiwa kwa muda wa miezi miwili mpaka pale taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Kaimu Afisa Afya wa Mwanza, Sophia Kiluvia, alisema TFDA imefanya kazi kubwa kuokoa uhai wa binadamu.
Alisema katika kipindi hiki kumeongezeka kwa viwanda bubu vingi vinavyoweza kuhatarisha maisha ya binadamu, hivyo kama serikali wana wajibu wa kushirikiana na wananchi kuhakikisha wanatokomeza tatizo hilo.