Kifo cha Filikunjombe, Paroko akitilia shaka


Wakati Rais Jakaya Kikwete, jana akiwaongoza viongozi wa serikali wakiwamo mawaziri, wabunge, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na waombolezaji mbalimbali waliojitokeza kuuaga mwili wa aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Ludewa, Deogratias Filikunjombe na wenzake wawili, Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Epifania Kijichi, Padri Respis Mzena, amehoji endapo kifo hicho ni mpango wa Mungu kweli ama la.  

Akiongoza ibada ya mwisho ya kuiombea miili ya marehemu hao iliyofanyika nyumbani kwa Filikunjombe Kijichi jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kwenda Ludewa Njombe kwa ajili ya maziko leo, Padri Mzena, alisema marehemu aliishi maisha ya useminari aliyohamia nayo uraiani.

Pia alihoji sababu ya kutokea kwa vifo mfulululizo wakati wa kipindi hiki cha uchaguzi mkuu na kuwataka Watanzania kumuomba Mungu pamoja na kutenda mema wakati wote ili kujiandaa na safari ya milele.

“Najiuliza kwa nini wakati huu vifo hivi, je ni mpango wa Mungu kweli? Kuna wakati watu walifariki sana kwa ajali. 

Pia kuna wakati watu wenye ulemavu wa ngozi waliuliwa kikatili kwa kukatwa na mapanga, kifo kama hicho hatuwezi kusema ni mpango wa Mungu, hivyo tunapaswa kumuomba Mungu na kuajiandaa wakati wote,” alisema Padri Mzena na kuongeza:

“Nilisoma na Filikunjombe, maisha ya seminari ya kujali wenzake na kupenda wengine, alijitoa kwa ajili ya wengine hasa wananchi wa jimbo lake na amekufa na rafiki zake ambao wakati wote aliwapenda,” alisema Padri Mzena.

Alitolea mfano kuwa, endapo CCM ingekuwa na wabunge wachapakazi kama, Filikunjombe ni wazi kuwa serikali kwa maana ya nchi ingepiga hatua kubwa ya maendeleo.

“Kwa sababu wema hawadumu, tunatakiwa kutenda mema bila kuchoka na kuamini kuwa watu wanaokufa katika mema wanaishi milele. 

Pia tusifikiri kuwa mtu anayekufa kifo cha mateso kama ndugu zetu hawa wametenda maovu, si kweli, tujiandae kwa kila wakati kutwaliwa,” alisema.

Miili iliyoagwa jana katika viwanja vya Hospitali ya Jeshi Lugalo, kabla ya kusafirishwa kuelekea nyumbani kwao Ludewa mkoani Njombe, ambayo inatarajiwa kuzikwa leo ni Filikunjombe, kaka yake, 
Plasdus Haule na rafiki yake, Egid Nkwera, ambao walifariki pamoja katika ajali ya Chopa iliyotokea Oktoba 15, mwaka huu.

Filikunjombe na wenzake wanne, akiwamo Rubani wa helikopta hiyo, Willium Silaa, walipoteza maisha katika ajali hiyo, iliyotokea mbuga ya Selous eneo la Msolwa mkoani Morogoro wakati wakisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Ludewa, Njombe.

Viongozi wengine waliojitikeza kuiaga miili hiyo ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Spika wa Bunge, Anne Makinda, mgombea wa nafasi ya urais (CCM), Dk. John Magufuli, mawaziri na wabunge mbalimbali wakiwamo wa vyama vya upinzani.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo