Katika hali isiyokuwa ya kawaida Raia mmoja wa Kichina amekutwa akihifadhi na kukausha viungo nyeti vya ng'ombe dume na baadaye kuhifadhi kwenye magunia, hali iliyosababisha harufu kali katika eneo hilo la makazi ya watu lililopo Tabata Bima jijini Dar es salaam.
Kubainika kwa Kiwanda hicho bubu cha kukausha viungo hivyo vya ng'ombe dume kumetokana na malalamiko ya wananchi wa eneo hilo, hususan wamiliki wa shule ya awali ya Cilos ambayo inapakana na kiwanda hicho .
Wakizungumza nasi, baadhi ya walimu katika shule hiyo wamesema wamekuwa wakisumbuliwa na harufu kali inayotoka katika eneo hilo ambayo imekuwa ikisababisha kukohoa mara kwa mara na maumivu ya vichwa hasa kwa watoto katika eneo hilo.
Wamesema kwa kipindi kirefu shughuli za kukausha viungo hivyo zimekuwa zikifanyika huku baadhi ya maafisa wakifika eneo hilo na kuondoka bila kuchukua hatua zozote dhidi ya kiwanda hicho bubu kilichopo makazi ya watu.
Baadhi ya watu wanaoleta bidhaa hizo na kuziuza kwa Mchina huyo wamesema hawaelewi kinachoendelea ingawa viungo hivyo nyeti vya ng'ombe wa kiume huanikwa na kukauka na baadaye kuhifadhiwa na kuondoshwa na magari katika eneo hilo.
Mfanyakazi wa kichina ambaye alikutwa katika eneo hilo hakutaka kuzungumza na waandishi wa habari na kudai kuwa bosi wake ambaye yuko eneo la Kariakoo ndiye msemaji.
Afisa mtendaji wa Eneo la Tabata Bima jijini Dar es salaam, Eligius Mulokozi amesema hana taarifa kuhusu shughuli zinazoendelea katika eneo hilo na kuahidi kulishughulikia.
